Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemwachia kwa dhamana mgombea Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Hashim Rungwe.
Mwanasiasa huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), alishikiliwa kwa siku nne akituhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa leo Septemba 6 amesema Rungwe ambaye pia ni mwanasheria aliachiwa kwa dhamana jana usiku kutokana na siku alizokaa mahabusu kuwa nyingi.
Mambosasa amesema pia wamejiridhisha kuwa hawezi kutoweka hata akiachiwa kwa dhamana.
“Tumejiridhisha kuwa wakili huyo mkongwe hawezi kutoroka amedhaminiwa na watu wa kuaminika na kwa kipindi hiki ataendelea kuripoti polisi kila atakapohitajika,” amesema.
Mambosasa amesema Rungwe akiwa wakili anatuhumiwa kushiriki kufanya udanganyifu kwa mfanyabiashara kutoka Uturuki, Suleiman Ysian ambaye alikuja nchini kununua korosho tani 15 kutoka kampuni ya Les Tropiques Group Mining Sprl Limited.
Amesema mkataba wa ununuzi wa korosho unaonyesha una gharama ya Dola 72,000 za Marekani sawa na Sh161 milioni ambazo zitalipwa kupitia akaunti ya benki ya wakili Rungwe.
Kamanda Mambosasa amesema inadaiwa mfanyabiashara huyo ameshalipa takriban Sh75 milioni lakini hakuna mzigo ulionunuliwa.