JESHI la Polisi Kanda Maalumya Dar es Salaam linamshikilia Robson Isack Maji (22) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Usimamizi wa fedha IFM na baba yake mzazi kwa kukamatwa na bastola aina ya Beretta na risasi sita.
Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa, Kamanda wa Polisi kandi hiyo, Lazaro Mambosasa amesema kuwa kijana huyo alikamatwa Septemba 20 majira ya saa 2:30 usiku maeneo ya mwenge akiwa katika harakati za kutaka kuikodisha bastola hiyo.
“Siku ya tukio, askari walipata taarifa na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea. Alikamatwa akiwa na bastola aina ya Berretya yenye namba DAA316502 ikiwa na risasi sita ndani ya magazine.
“Mwanafunzi huyo alikuwa akitaka kukodisha silaha hiyo kwa majambazi kwa gharama ya Tsh. 400,000 lakini pia alikuwa tayari kuiuza kwa Tsh. Milioni 2,500,00.
“Kwa mahojiano ya awali na mtuhumiwa huyo ilibainika kuwa silaha hiyo aliiba kwa baba yake aitwaye Isack Maji ambaye naye siye mmiliki halali wa silaha hiyo. Kwa hiyo, baba na mtoto wote tunawashikilia ili watuambie waliitoa wapi silaha hiyo,” alisema Mambosasa.