Jeshi la Polisi Limekanusha Taarifa za Askari Wao Kuhusishwa Kwenye Tukio la Kuvamiwa Lissu

Jeshi la Polisi Limekanusha Taarifa za Askari Wao Kuhusishwa Kwenye Tukio la Kuvamiwa Lissu
MSEMAJI wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa, amekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii zikionyesha picha za polisi kuhusika na shambulio lililomjeruhi kwa risasi Mbunge Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mwakalukwa amesema kuwa taarifa hizo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii Septemba 11 mwaka huu, hivyo jeshi la polisi limekanusha taarifa hizo kuwa ni za uongo na zenye lengo la kumchafua askari huyo na jeshi la polisi kwa ujumla.

“Askari huyo hayupo Nairobi kama ilivyoenezwa na picha iliyotumika mitandaoni, picha hiyo ilipigwa hapa nchini Januari 7 mwaka huu ambapo askari wetu alikuwa kwenye sherehe ya mahafali ya mtoto wa kaka yake.

“Kuhusiana na safari ya Nairobi, askari huyo alikuwa nchini Kenya kwa kozi ya kimafunzo kuanzia Septemba 4 hadi 8 mwaka huu aliporejea Tanzania baada ya mafunzo na kuongeza kwamba Tundu Lissu alipelekwa nchini Kenya usiku wa Septemba 8 mwaka huu baada ya kupatwa na mkasa huo wa kujeruhiwa kwa risasi,” alisema Mwakalukwa.

Mwakalukwa alisema kwamba jeshi la polisi limekemea vikali kitendo hicho chenye lengo la kumharibia maisha yake askari wao na ametoa onyo kwa wote wanaofikiri kuwa wanaweza kukaa na ‘kupika habari’ ili waweze kuivuta jamii iwe upande wao na kuchafua upande wa serikali.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad