"Kama unajijua uli-comment chochote kuhusu taarifa hiyo njoo mwenyewe kabla hujatafutwa, tuna njia zetu tunaweza kuwafikia," amesema Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alipozungumza na waandishi wa habari leo Jumanne.
Jeshi la Polisi limekanusha taarifa hizo zilizosambaa tangu jana Jumatatu kwenye mitandao ya kijamii zikihusisha picha ya askari huyo.
Mwakalukwa amesema taarifa hizo hazina ukweli kwa kuwa kachero huyo alikuwa Nairobi kwa mafunzo maalumu na tayari amesharejea nchini.
"Askari huyo alikuwa nchini Kenya kwa kozi ya mafunzo kuanzia Septemba 4 hadi Septemba 8, wakati Lissu alijeruhiwa Septemba 7," amesema.
Mwakalukwa amesema, "Tunatoa onyo kwa wote wanaofikiri wanaweza kukaa na kupika habari ili waweze kuivuta jamii iwe upande wao na kuchafua upande wa Serikali."
Amesema polisi kupitia kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao inaendelea na uchunguzi kuwabaini wanaohusika kusambaza taarifa za uongo.
Mbunge Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) alijeruhiwa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma, Alhamisi Septemba 7.
Baada ya shambulizi hilo lililotekelezwa na watu wasiojulikana alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Aga Khan mjini Nairobi, Kenya.