Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limeitaka Serikali ifanye mabadiliko ya msingi katika Katiba kabla ya kuingia kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.
Jukata imesema mabadiliko hayo ya msingi yafanyike iwapo hakuna uwezekano wa kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020, kama ambavyo dalili zinazidi kuonyesha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukata, Hebron Mwakagenda amesema kwa hali ilivyo dalili ya kupatikana Katiba Mpya hakuna, kutokana na kutotengwa bajeti kwa ajili ya mchakato huo.
Amesema ipo haja ya kurekebisha angalau mambo ya msingi ambayo yamelalamikiwa na wananchi kwa kipindi kirefu.
Amesema kutokana na hilo yafanyike mabadiliko muhimu katika Katiba iliyopo ikiwamo kuwapo na uhuru kamili ya tume ya uchaguzi Zanzibar.
Aliyataja mabadiliko hayo ni kuwa na uhuru kamili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Amesema mabadiliko hayo pia yaangalie kuwapo kwa fursa ya mgombea huru katika uchaguzi, ikiendana na kutokuwa na masharti makali yanayokatisha tamaa.
Amesema pia Katiba ibadilishwe na iwe na nafasi ya kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani na pia kuwezesha vyama vya siasa kuungana kikatiba na kisheria kwa lengo la kusimamisha mgombea mmoja.
“Hili siyo la vyama vya upinzani pekee, hata chama tawala CCM itafikia mahali kitahitaji kuungana na vyama vingine kusimamisha mgombea mmoja."
“Siasa zinabadilika sana na chenyewe ni kama kipo ukingoni, hivyo hili liangaliwe na lipewe nafasi kwenye Katiba,” amesema Mwakagenda.
Aliyataja mabadiliko mengine ni kurejesha mfumo wa ushindi katika uchaguzi wa Rais kwa kigezo cha kupatikana kwa kura zisizopungua 50 jumlisha moja