Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Septemba 28, 2017, Kamanda Msilimu amesema Jeshi hilo kwa kufuata maagizo ya Rais John Magufuli limeamua kufanya oparesheni kali usiku na mchana kuwabaini, kuwakamata na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafungia leseni madereva wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani lengo ikiwa ni kupunguza ajali na vifo ambavyo vimekuwa vikitokana na ajali hizo.
“Watu wamezoea oparesheni zetu mchana, kwa sasa tunafanya hadi usiku kwa maana tochi zetu zinakamata muda wowote, kwa hiyo sisi tutapambana nao muda wote. Tumeanza na Dumira na sasa tunaendesha oparesheni hii mikoa yote na barabara zote nchini.
“Kwa kipindi cha wiki moja ambacho oparesheni imeanza tarehe 14-18, Septemba 2017, tumekamata jumla ya makosa 53,870, tumekamata madereva saba wa mabasi makubwa yakiwa yanaendehswa kwa mwendo mkali wa Kilometa 90 kwa saa tena usiku. Baada ya kukamatwa tuliwapeleka mahakamani na wakakiri makosa yao. Kwa mujibu wa sheria ninatangaza kuwafutia leseni zao wote.
“Taarifa zao tumezipeleka TRA, SUMATRA na kwa wamiliki wa mabasi (TABOA), iwapo watahitaji kuendelea na kazi hiyo, watatakiwa kukaa kwa miezi sita kisha warudi darasani wakasome, wakifaulu waje tuwatahini hadi tujiridhishe kuwa wameiva ndipo tuwarejeshee madaraja yao ya leseni,” alisema Musilimu.
Madereva waliofutiwa leseni zao ni Hamad Shabani Salum (leseni namba 4001852854), Kija Aloyse Mayenga (leseni namba 4001518000), Isack John Mbijina (leseni namba 4000220395), Hassan Abbas Semazua (leseni namba 4001522366), Stanley Joseph Mosha (leseni namba 4000369436), Abdallah Hussein (leseni namba 4000482412) na Sempunda Yusuph (leseni namba 119808006515226).
Wengine waliofungiwa leseni zao ni madereva waliosababisha ajali mbalimbali hivi karibuni ambao ni; Isamil Mohammed Nyami, Mseka Herman Salum, Marick Hamidu Hassan ambao hawatakaruhusiwa kuendesha magari ya abiria. Kamanda Musilimu pia amefungia mabasi 11 ya abiria kwa kukiuka taratibu za usafirishaji kwa njia ya barabara.