Kampuni ya Ukamataji wa Magari Dar Yafutiwa Mkataba

Kampuni ya Ukamataji wa  Magari Dar Yafutiwa Mkataba
Meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amefuta mkataba wa kampuni ya ukamataji wa magari Mwamkinga Auction Mart kwa kile kilichodaiwa amekuwa ikifanya kazi kwa kutozingatia matakwa ya mkataba ikiwemo kuwatoza watu faini  kuanzia Sh 200,000 hadi Sh 300,000.

Mwita amesema halmashauri ya jiji iliingia mkataba na kampuni hiyo Aprili 1 mwaka huu ili kudhibiti uegeshaji wa magari katika maeneo yasiyo rasmi yaliyopo katika Manispaa ya Temeke na Kigamboni.

Amesema halmashauri hiyo ilifuatilia kwa karibu utendaji wa kazi wa kampuni hiyo baada ya kupata malalamiko ya wananchi na kujidhihirisha kwa ushahidi uliojitosheleza kuwa ilikuwa ikifanya kazi kwa kutozingatia mkataba waliokubaliana nao.

"Mkataba wake tumesitisha kuanzia Septemba 19 mwaka huu na nimesikia bado wapo barabarani wanakusanya hizo faini hivyo hawatakiwi kuonekana na wakiendelea watachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Mwita.

Mwita amesema kampuni hiyo inatakiwa kuondoka kwenye maeneo waliyopangiwa kufanya kazi hiyo na kuhakikisha inakabidhi mashine zote za kukusanyia mapato ya halmashauri hiyo zikiwa katika hali nzuri.

Amesema haiwezekani mtu amesimama kwa dakika moja unafunga gari lake kwa mnyororo na kumwandikia faini ya Sh 200,000 hadi Sh 300,000 ambayo haipelekwi kwenye halmashauri hiyo.

“Hiyo kampuni ilikuwa inafanya kazi hadi saa tatu usiku tofauti na makubaliano ya mkataba unavyosema mwisho saa 12 jioni.”

Amesema anaendelea kufuatilia kwa Wilaya ya Kinondoni na Ilala  ambapo kama wataenda tofauti na mikataba inavyosema watasitishwa mikataba yao.

Mwita amesema lengo la halmashauri hiyo siyo kumkandamiza mwananchi bali kusimamia sheria ili watu wazifuate lakini imeonekana tofauti.

 "Na nimesikia wanakusanya hadi shilingi milioni nne kwa mwezi ambazo haziwasilishwi hapa halmashauri ya jiji,” amesema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad