Kikosi Maalum cha Kupambana na Matukio ya Mashambulio ya Risasi Kuanzishwa na Serikali

Kikosi Maalum cha Kupambana na Matukio ya Mashambulio ya Risasi Kuanzishwa na Serikali
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa imesema imepanga kuunda kikosi maalum kitakachohusisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama ili kupambana na matukio ya kihalifu ikiwemo mashambulio yanayohusisha silaha za moto

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi leo bungeni wakati alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Mkoani (CUF) Twahir Mohamed alipouliza ni kwa nini Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lisihusishwe katika kukomesha matumizi ya silaha na mauji ya raia wasiokuwa na hatia yeyote nchini huku akitolea mfano kwa tukio la shambulio la Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mirataba pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ambao wote walishambuliwa na risasi katika siku tofauti ndani ya mwezi huu.

Waziri Mwinyi amesema hapana shaka kuwa kazi ya Jeshi la ulinzi ni kulinda mipaka ya nchi, lakini pale linapohitajika kutoa msaada katika maeneo mengine, chombo hicho kipo tayari kufanya hivyo.
"Ni dhahiri kwamba kazi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania( JWTZ) ni kulinda mipaka, lakini pale ambapo linahitajika au linaombwa kusaidia mamlaka nyingine, iwe za kiraia au iwe vyombo vingine vya ulinzi na usalama, basi wanakuwa tayari kufanya hivyo", amesema Dkt. Mwinyi.

Pamoja na hayo, Waziri Mwinyi ameendelea kwa kusema "Kwa hali ilivyo sasa itaundwa 'task force' (kikosi maalumu) itakayojumuisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama, ili kuweza kulifanyia kazi tatizo hili la uvunjifu wa amani ndani ya nchi na sina shaka juu ya kazi hiyo kwa kuwa naamini imeshaanza", amesisitiza Waziri Mwinyi.
Kwa upande mwingine, Dkt. Mwinyi amewahakikishia Watanzania na kusema jukumu hilo litatekelezwa mapema ili hali ya usalama ipatikane ndani ya nchi.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad