Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika na mwanaharakati wa haki za wanawake nchini, Balozi Getrude Mongella amesema moja ya ndoto zake ilikuwa ni kupata watoto 12.
Akitoa simulizi ya namna alivyofanikiwa kutimiza ndoto zake katika tamasha la Jinsia la 4, lililofanyika kwenye viwanja Mtandao wa Jinsia Tanzania, Mongella amesema ‘’kiuhalisia napenda watoto kwa sababu wanaufurahisha moyo wangu’’.
Amesema uzazi wa oparesheni ndiyo uliomfanya ashindwe kutimiza ndoto hiyo hata hivyo alipata watoto watatu.
Amewaambia wanachama wa TGNP waliokuwa wanamsikiliza kwa hamu kuwa mafanikio yake
kisiasa yanatokana na malezi mazuri ya wazazi wake.
“Baba yangu alipenda kuona natimiza ndoto zangu, alinisapoti kila hatua na nilipokuwa nafanya mikutano alikuwa ananisikiliza na kunipongeza ninapofanya vizuri,”anasema
Siri ya mafanikio ni kujiamini, kujituma na kuthubutu.“Hata kama roho inauma, nilijipa ujasiri nikathubutu,”anasema.