MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ametokea benchi usiku wa Jumamosi timu yake, KRC Genk ikifungwa 2-1 na mahasimu, Sint-Truiden katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji uliofanyika Uwanja wa Stayen mjini Sint-Truiden, St.-Trond.
Samatta aliingia dakika ya 73 kuchukua nafasi ya mshambuliaji kinda wa umri wa miaka 21, Mdenmark, Marcus Ingvartsen dakika ya 73 wakati huo timu hazijafungana.
Lakini baada ya Nahodha wa Tanzania kuingia, Genk ikafungwa mabao mawili ya haraka haraka ndani ya dakika tano, kwanza Roman Bezus dakika ya 78 na baadaye Damien Dussaut dakika ya 83, kabla ya Siebe Writers kuifungia bao la iufutia machoi dakika ya 88.
Huo unakuwa mchezo wa 62 kwa Samatta katika mashindano tangu Januari mwaka jana alipojiunga na Genk, kati ya hiyo mechi 36 alianza na mechi 23 ametokea benchi.
Katika mechi hizo, mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon, zamani Mbagala Market na Simba zote za Dar e Salaam, amefunga jumla ya mabao 21.
Kikosi cha STVV kilikuwa: Lucas Pirard, Stelios Kitsiou, Jorge Teixeira, Sascha Kotysch, Casper de Norre/Dussaut dk80, Igor Vetokele/Jordan Botaka dk67, Charilaos Charisis, Steven De Petter, Jonathan Legear/Roman Bezus dk67, Yohan Boli na Alexis De Sart.
KRC Genk: Danny Vukovic, Joakim Mæhle, Omar Colley, Jakub Brabec, Jere Uronen, Ruslan Malinovskiy/Bryan Heynen dk88, Sander Berge, Alejandro Pozuelo, Thomas Buffel/Edon Zhegrova dk73, Marcus Ingvartsen/Mbwana Samatta dk73 na Siebe Writers.