Mbunge wa Ubungo (Chadema) Saed Kubenea amesema aliugua ghafla akiwa njiani kuelekea katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Amesema aliitikia wito wa Spika Job Ndugai ambaye Jumanne wiki hii alimpeleka mbele ya kamati hiyo.
Spika alisema Kubenea anamtuhumu kwenye mitandao ya kijamii kuwa amesema uongo kuhusu idadi ya risasi alizopigwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Kubenea amesema alitakiwa kuripoti mbele ya kamati saa 7:30 mchana lakini alipokwenda aliambiwa kuna shughuli za Bunge zimeingiliana hivyo arejee saa 9:30.
Mbunge huyo amesema hakuweza kurejea mbele ya kamati baada ya kuugua ghafla.
“Nilishaenda kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, wakati ninakwenda kwa Kamati ya Maadili nikapata
tatizo,” amesema Kubenea.
Awali, Katibu wa Wabunge wa Chadema, David Silinde alisema Kubenea alikwenda kwenye zahanati ya Bunge baada ya kujihisi vibaya.
“Alijisikia kukosa nguvu akaenda zahanati, amepumzishwa na sasa anasema ni simu yake ya kwanza kuongea nayo tangu
apumzishwe. Ndiyo amekaribia kumaliza dripu,” alisema Silinde.
Daktari wa zahanati ya Bunge, Noel Solomoni alithibitisha kupumzishwa kwa mbunge huyo tangu saa kumi jioni.
Mwananchi: