Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesafirishwa kwa ndege leo Jumatano asubuhi kwenda Dodoma anakohitajika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
"Sasa hivi nipo bungeni nasubiri Kamati ya Maadili nimefika tangu saa moja asubuhi kwa ndege," amesema Kubenea.
Mbunge huyo jana Jumanne alisema alikuwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay wilayani Kinondoni akisubiri utaratibu wa safari hiyo ya kwenda kuhojiwa kama Spika wa Bunge Job Ndugai alivyoagiza.
Katibu wa wabunge wa Chadema, David Silinde akizungumzia safari ya mbunge huyo amesema, "Kweli amesafirishwa kwa ndege leo asubuhi kwenda Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa na kamati. Huu ni upotevu wa rasilimali za umma kwa shughuli ambayo ingeweza kufanywa hata kwenye kikao kijacho cha Bunge," amesema.
Amesema kutojitokeza mbele ya kamati kwa mbunge huyo tangu alipoitwa kunatokana na afya yake na hata jana Jumanne alipokamatwa alichukuliwa akiwa hospitali.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kusafirishwa mbunge huyo amesema hana taarifa mpya lakini alitakiwa kuondoka leo asubuhi kwa ndege.
Kubenea alisema jana kuwa, kabla ya kushikiliwa alikwenda kujisalimisha polisi katika kituo cha Oysterbay na aliambatana na askari hadi katika Hospitali ya Aga Khan ambako alitakiwa kwenda kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha MRI.
Kubenea amepelekwa mbele ya kamati akituhumiwa kwa taarifa alizozitoa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Spika alisema uongo kuhusu idadi ya risasi alizopigwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu katika tukio lililotokea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba 7