Lema amesema hayo leo alipokuwa jijini Arusha akiongea na waandishi wa habari na kusema amesikitishwa sana na majibu ya Waziri Mwigulu Nchemba kuhusu sakata la miili ya watu kuokotwa baharini na sakata la shambulio la Tundu Lissu pamoja na kupotea kwa Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
"Mwigulu Nchemba amenisikitisha sana kwa kauli zake alizokuwa anatoa na sidhani kama anastahili kukalia ile ofisi hata kwa masaa 12 na ni wito wangu kwa Mhe. Rais Magufuli na naamini itakuwa hivyo hawezi kumuacha Waziri kama huyu kwenye ofisi ya serikali inayoshughulika na mambo ya ulinzi na usalama wa watu, matumaini yangu yupo hapo kwa muda tu, toka utamaduni wa maiti za watu kuanza kuokotwa zimeokotwa maiti za watu wengi sana lakini unaona kauli ya Waziri ni kama watoto wameokota maembe, amesema hawana mpango wa kuleta wachunguzi kutoka nje kuja kusaidia polisi kuchunguza tukio la Tundu Lissu hiyo ni hofu sababu wanajua nini kipo nyuma ya jambo hilo" alisema Lema
Aidha Mbunge huyo amesema kuwa kitendo cha Waziri Mwigulu Nchemba kusema gari ambayo alikuwa anailalamikia Mbunge Tundu Lissu na yeye kusema gari hiyo imeonekana Arusha na haijawahi kutoka Arusha bila kuchukuliwa hatua yoyote ni jambo ambalo linaibua maswali mengine na kufanya wazidi kukosa imani na jeshi la polisi kuhusu kuchunguza sakata la Tundu Lissu.
"Gari ikiwa inatuhumiwa Waziri hasemi kuwa gari hiyo imeonekana Arusha na haijawahi kutoka Arusha ila gari ikiwa inatuhumiwa cha kwanza watu wanatakiwa kuwajibika lakini ukweli ni kwamba watu wanatumia namba feki kwa ajili ya matukio, jana Waziri anaongea vitu vyepesi mimi nasema siku za Waziri huyu kukaa pale kama Waziri wa Mambo ya Ndani siku zake zinahesabika na nyinyi mtaniambia, anasema hajui kama Ben Sanane amekufa au hajafa kama mpaka leo Waziri wa
Mambo ya Ndani hajui juu ya Ben Sanane kama amekufa au yuko hai polisi hawa tunasema hawawezi kuchunguza sakata la shambulio la Tundu Lissu ndiyo maana tunataka uchunguzi kutoka nje ya nchi waje kusaidia jambo hili" alisema Godbless Lema