Mbunge wa Arusha Mjini ambaye sasa yupo nchini Kenya amewaomba Waziri wa Mambo ya Ndani na IGP Sirro wawaachie watu ambao jana walikamatwa na jeshi la polisi wakiwa wamevaa Tshirt za Tundu Lissu na UKUTA na kusema kitendo hicho kinazidi kuleta chuki.
Lema amesema hayo kupitia mitandao yake ya kijamii na kudai kuwa watu ambao wameratibu maombi kwa ajili ya Tundu Lissu hawakupaswa kukamatwa bali walipaswa kulindwa na jeshi la polisi kwani wao wanaratibu watu waweze kumlilia Mungu wao kwa maombi na si vinginevyo.
"Hivi kweli hawa watu wangekuwa wanafanya mkusanyiko wa maombi kwa ajili ya Rais Magufuli au kiongozi mwingine yoyote yule hawa watu wangepata mateso makubwa kama ambavyo wale vijana wamepata, Mwigulu Nchemba wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Kamanda Sirro tunakuomba sana waachie watu wote waliokamatwa wakiwa wamevaa Tshirt za UKUTA waachie kwa sababu hiki mnachokifanya kikiendelea kukomaa siku moja hamtawaona na Tshirt wala na kitu chochote wakiacha kuvaa Tshirt mioyo yao ikaendelea kuumia wakiacha kusali maana yake watakuwa wameelekea katika njia nyingine mbaya zaidi" alisisitiza Gobless Lema
Godbless Lema ametoa kauli hii siku moja baada ya jeshi la polisi kuzuia watu kufanya maombi ya kitaifa kwa Mbunge Tundu Lissu maombi ambayo yaliandaliwa na vijana wa CHADEMA (BAVICHA) ambayo yalipaswa kufanyika Septemba 17, 2017 katika viwanja vya TIP Sinza l Rights