Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola ametoa wito huo alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tuhuma za rushwa zilizotolewa na wabunge hao.
Jumamosi iliyopita, Diwani wa Kimandolu (Chadema), Mchungaji Rayson Ngowi alitangaza kuihama Chadema na kujiunga na CCM wakati wa tukio la Rais Magufuli kutunuku kamisheni kwa maofisa 422 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jijini Arusha.
Katika tukio hilo, Rais Magufuli aliuliza kama kuna mwanachama yeyote anayetaka kujiunga na chama hicho au kukihama, ajitokeze mbele na ndipo diwani huyo alijitokeza na kutangaza rasmi kujiunga na CCM kwa maelezo ya kuvutiwa na utendaji wa Serikali.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo, Nassari ambaye ni Mbunge wa Chadema wa Arumeru Mashariki, alizungumza na waandishi akiwaeleza kwamba ana ushahidi wa kielektroniki unaoonyesha madiwani hao walivyopewa rushwa ili wajiuzulu nafasi zao.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Mlowola alisema, “Bado hawajatuletea ushahidi wowote lakini tunasubiri watuletee, hakuna shida maadam wamesema hivyo, tunawakaribisha.”
Wakizungumzia uamuzi wa Mlowola kuwasubiri wabunge hao badala ya kuwafuata baadhi ya wachambuzi wamesema ni uamuzi sawa lakini hawaamini kama Takukuru wangependa Rais Magufuli achafuliwe.
Profesa George Shumbusho kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema haoni tatizo lolote kwa wabunge hao kuwasilisha ushahidi walionao kwa Takukuru.
“Sioni shida wakipeleka kama wanao kweli, halafu wao Takukuru ndiyo wataupima ushahidi huo, wakikabidhi Takukuru ndiyo wanaweza kusema hadharani sasa,”
“Nadhani hawajawafuata pengine wanaamini ni tuhuma za kisiasa tu,” alisema.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Gemma Akilimali alisema hakuna haja ya Takukuru kuhangaika kuanza kazi ya uchunguzi wakati ushahidi umeshapatikana kwa wabunge hao.
Alisema ni vyema wakapeleka ili kurahisisha kazi kwa chombo hicho.
“Kama wangesema tuna wasiwasi wa kuwapo mazingira ya rushwa na wangeiomba Takukuru ichunguze lakini sasa wameshasema ushahidi wanao tayari, kwa hiyo wapeleke ili ionekane kama ni uongo au ni ushahidi wa ukweli,” alisema Gemma.
Siku ya tukio wakati Mchungaji Ngowi anapokelewa na Rais Magufuli alisema madai ya rushwa hayana ukweli wowote na kama Nassari ana ushahidi ni vyema angeutoa hadharani.
Ngowi aliwashauri Chadema mkoani Arusha watatue matatizo yaliyopo ndani ya chama hicho na wasitafute visingizio kwa kuwa yeye ameamua kujiuzulu kwa kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na hajapewa rushwa yoyote.
Madiwani wengine waliojiuzulu chama hicho ni Credo Kifukwe wa Kata ya Murieti jijini Arusha, Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu) Solomon Laizer (Ngabobo).
Mmoja kati ya hao waliojiengua, Credo Kifukwe alisema hakuna chochote alichopewa kama rushwa kwa lengo la kujiuzulu, akimshauri Nassari autoe hadharani ushahidi anaousema na si kushusha tuhuma zisizo na mashiko.
Katika ufafanuzi wake, Nassari aliyekuwa ameongozana na Lema alisema ushahidi huo ameuhifadhi ndani ya ‘flash disc’ na yuko tayari kumkabidhi Rais Magufuli na vyombo vya uchunguzi.
Mbunge huyo alisema endapo ikithibitika kuwa ushahidi wake ni wa uongo yuko tayari kujiuzulu nafasi yake ya ubunge.
“Ninao ushahidi na kama Mheshimiwa Rais yuko tayari niko tayari kumpatia ninayo flash, ushahidi ninao kwa muda mrefu na tulijua watapokelewa juzi madiwani wawili lakini mmoja amekataa akaenda mmoja,” alisema Nassari.