Mbunge wa Kilombero mkoani Morogoro, Peter Lijualikali ameshikiliwa na kuhojiwa na polisi wilayani Malinyi kwa saa nne.
Pamoja naye, viongozi wengine watatu wa Chadema walishikiliwa jana Alhamisi wakidaiwa kufanya mkusanyiko bila kuwa na kibali cha polisi.
Akizungumza leo Ijumaa baada ya kuachiwa mbunge huyo amesema aliamriwa na polisi kusimama alipokuwa akitoka kwenye kikao cha ndani cha viongozi na baadhi ya wanachama wa Chadema katika Kijiji cha Makerere wilayani Malinyi.
“Nilipoamriwa kushuka kwenye gari nilitii na kuongozana na polisi hadi kituo cha i Malinyi ambako nilihojiwa kwa nini nifanye kikao bila kibali. Nikawaambia kilikuwa ni kikao cha ndani wakasisitiza kuwa ni lazima tuwe na kibali,” amesema Lijualikali.
Amesema hakuna sheria inayowataka kuwa na kibali wanapofanya vikao vya ndani kwa kuwa hawahitaji ulinzi wa polisi katika vikao hivyo na hapakuwa na uwezekano wa kutokea vurugu.
Mbunge huyo amesema alipoona anahojiwa muda mrefu aliamua kumpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei aliyemweleza yupo likizo.
Amesema aliamua kumpigia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na kumweleza kilichotokea ambaye aliahidi kushughulikia suala hilo.
“Nashukuru baada ya kuongea na Mwigulu niliachiwa. Niliondoka kituoni hapo saa nne usiku tangu wanishikilie saa 12:00 jioni. Walinitaka kuripoti kesho yake (leo) saa mbili asubuhi na niliripoti wakaniambia niripoti tena Oktoba 5,” amesema.
Wengine waliokamatwa pamoja na mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Chadema Malinyi, Emmanuel Lukindo; Katibu wake, Sadi Lyampawe na Katibu Mwenezi wa wilaya, Lucas Lyambalimu ambao wote wameachiwa kwa dhamana.