Alikiba ambaye sasa anafanya vyema na wimbo wake 'Seduce me' amefunguka na kusema kuwa lugha ya Kiswahili si kikwazo kwake na muziki wake kufika kimataifa na kusema yeye anajivunia kutumia lugha hiyo ambayo kwa sasa ni kati ya lugha kubwa duniani.
Alikiba alisema hayo alipokuwa akihojiwa kwenye kipindi cha eNewz wiki kadhaa zilizopita na kusema anajisikia fahari kutumia lugha ya Kiswahili katika muziki wake na kusema kufanya hivyo inasaidia pia kukuza lugha yetu ya Kiswahili ulimwenguni.
"Hakuna kizuizi cha lugha kwenye muziki zamani tulikuwa tunapenda miziki ya Kiringala lakini tulikuwa hatujui nini wanaimba, tulikuwa tunapenda miziki kutoka Congo lakini hatuelewi wanaimba nini na bado mpaka sasa kuna watu wanapenda miziki ya kizungu lakini hawaelewi kizungu hivyo hakuna kizuizi cha lugha kwenye muziki. Kiswahili ni lugha kubwa Afrika na ni lugha ambayo inaheshimika sana barani Afrika na tunapoendelea kuimba Kiswahili tunaikuza lugha yetu kwanza mimi najivunia kuwa Mswahili nasaidia kukuza lugha yetu ya Kiswahili ifike kote inapotakiwa kufika kwa sababu tayari ni lugha kubwa duniani" alisema Alikiba
Aidha Alikiba aliendelea kusema kuwa kwa sasa sehemu ambazo anakwenda kufanya matamasha yake nje ya Tanzania mashabiki wamekuwa wakiimba nyimbo zake hizo japo si kwa kupatia lakini ni hatua kuwa wanapenda anachoimba licha ya kutoelewa maana yake na kudai hiyo ni njia moja wapo ya kuzidi kukuza lugha ya Kiswahili.
"Kuimba Kiswahili hakukwamishi kabisa muziki wetu kufika mbali kinachotakiwa kufanya muziki mzuri tu, mimi nishafanya matamasha mbalimbali nje ya Tanzania mfano Finland sikuwaimbia tu wabongo au Wakenya, nishafanya matamasha Oman na sehemu zingine watu wanaimba wewe hawajali yaani, Wanaigeria wanaimba ngoma zangu mimi, wanaimba japo hawapatii kabisaa lakini wanahisi nimeimba vizuri ndiyo maana wanapenda na kuimba na mimi" alisema Alikiba