Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Mh.Wilfred Lwakatare na mwenzake, Ludovick Rwezaura waliokuwa wakistakiwa kwa kosa la kula njama za kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru aliyekuwa Mhariri wa Gazeti.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amewaachia huru washtakiwa hao leo Alhamisi mara baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuomba kesi hiyo ifutwe chini ya kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai kisha Mahakama kuridhia.
Kishenyi ameomba kesi hiyo ifutwe chini ya kifungu hicho kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao na baada ya kutolewa kwa maelezo hayo hakimu aliwaachia huru washtakiwa hao leo.
Pamoja na hayo Mh. Lwakatare amemshukuru Mungu kwa kuwa na siku njema na yenye furaha.
Hata hivyo wakati kesi hiyo inaondolewa mahakamani hapo alikuwapo Mbunge Lwakatare pekee huku mshtakiwaRwezauraakiwa hajafika kwa kile kinachodaiwa kuwa na matatizo ya kifamilia.
Awali Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilimfutia kesi ya makosa ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph, baaadaye Jamhuri ilikata rufaa kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu.