Mahakamani: Ulikutwa Msokoto wa Bangi Kwenye Kabati la Vyombo Vya Wema

Mahakamani: Ulikutwa Msokoto wa Bangi Kwenye Kabati la Vyombo Vya Wema
Ofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Inspekta Wille ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alikuta msokoto wa bangi kwenye Kabati la vyombo la Wema Sepetu.

Inspekta Wille ameyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula kutoa ushahidi katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili Wema na wenzake.

Akitoa ushahidi wake Mahakamani hapo, alidai kuwa anakumbuka February 4, 2017 aliitwa na Mkuu wake wa kazi na kupewa jukumu la kufanya upekuzi nyumbani kwa Wema ambapo aliongozana na Maofisa wenzake pamoja na Wema hadi nyumbani kwa Wema Ununio.

Alidai baada ya kufika nyumbani kwa Wema walimkuta dada wa kazi ambaye walimuomba waonane na Mjumbe wa Shina la maeneo hayo.

”Mjumbe alifika na tulimwambia tunataka kufanya uchunguzi katika nyumba hiyo ili kutafuta dawa za kulevya.”

Shahidi huyo alidai kuwa kabla hawajaingia ndani, Wema aliomba wakati upekuzi unafanyika dada yake awepo na alipofika akawapeleka ndani.

”Tulianza kupekua jikoni, ambapo juu ya Kabati la vyombo tulikuta msokoto mmoja wa Bangi na Lizra. Pia tukaingia kwenye chumba cha Wema anapohifadhia nguo ambapo tukakuta msokoto mmoja unaodhaniwa ni Bangi juu ya dirisha.”

Aidha, amedai kuwa baada ya hapo walifanya uchunguzi ndani ya chumba cha wadada wa kazi ambapo walikuta msokoto wa Bangi uliotumika ndani ya Kibiriti na baadaye walijaza hati ya ukamataji, kisha kuondoka na Wema hadi Kituo cha Polisi.

”Hivyo, February 8, 2017 tulimpeleka Wema Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kufanya vipimo vya mkojo, tulivyomaliza vipimo tulikabidhi sampuli hiyo.”

Baada ya kuelez hayo, shahidi huyo aliiomba Mahakama ipokee kielelezo hicho cha ukamataji mbele ya Mahakama ambapo hata hivyo, Wakili wa utetezi Peter Kibatala alipinga kupokelewa kwa hati hiyo, akidai ina mapungufu kisheria.

Kutokana na mvutano huo, Hakimi Simba ameahirisha kesi hiyo hadi September 13, 2017 kwa ajili ya kutoà uamuzi wa kupokea kielelezo hicho ama la.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad