Majaliwa Azindua Mradi wa Maji Longido

Majaliwa Azindua Mradi wa Maji Longido
Baadhi ya wabunge wa CCM wameonekana kumpigia kampeni za chinichini aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Longido (CCM), Dk Steven Kiruswa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015 mbele ya Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa aliyekwenda kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Longido.

Juni 29, 2016, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitengua ushindi wa mbunge wa Longido, Onesmo Ole Nangole (Chadema) na sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inasubiriwa kutangaza kama liko wazi na tarehe ya uchaguzi.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha (CCM), Catherine Magige alitumia nafasi ya kusalimia wananchi aliyopewa na mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo kumtambulisha Dk Kiruswa na kusema amekuwa akimtuma bungeni kuzungumzia matatizo ya Longido.

“Yale ambayo nimekuwa nikiyazungumza bungeni kuiomba Serikali, huyu hapa (akimwonyesha) Dk Kiruswa ndiyo alikuwa ananiambia, kila siku ananisumbua kwenye simu. Yeye hakushinda ubunge lakini anatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia mimi,” alisema Magige.

Dk Kiruswa alisimama jukwaani na kuwasalimia wananchi na kuwaahidi kwamba hata umeme ambao wamekuwa wakiulilia wataupata.

Alisema, “…umeme pia nasikia mtaupata, nimekuwa nikiwasumbua kwa ajili ya vile vijiji ambavyo hakuna (umeme).”

Gambo aliwatambulisha wabunge wengine wa CCM akisema wamekuwa wakilizungumzia Jimbo la Longido katika kipindi chote cha mwaka mmoja ambacho wamekuwa hawana mbunge.

“Huu ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na nilipokuwa naongea mambo ya maji nilikuwa nafikiria Longido, nilikuwa nafikiria Mererani, nilikuwa nafikiria Orkesmet,” alisema Mary Nagu, mbunge wa Hanang’ alipokuwa akisalimia wananchi.

Naye mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Amina Mollel alisema kwa miaka miwili hawakuwa na mbunge, anaamini kwamba hawatafanya kosa tena kuchagua mtu mwingine.

“Dk Kiruswa oyeee! Huyu ndiye wa kwenu, hajaondoka popote, halafu ni dokta kwa kusoma vidato vyote hivyo. Hamjisikii kuwa na furaha, hamuoni kwamba akija kule anasaidia kutupika ili tuwe wanasiasa wazuri,” alisema Mollel wakati akisalimia wananchi.

Gambo naye alisisitiza kwamba Dk Kiruswa amekuwa akimsumbua kuhusu shida za wananchi wa Longido. “…kwa sababu mimi sina kinga kama za wabunge, mimi nawatakia kila la heri wananchi wa jimbo hili.”

Baada ya tambo na kampeni hizo za chinichini, Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alianza hotuba yake akisisitiza kwamba Serikali itahakikisha inakabiliana na changamoto zote katika Wilaya ya Longido ikiwamo uhaba wa maji.

Majaliwa alizindua ujenzi wa mradi wa maji wa Longido ambao unaanzia kwenye chanzo cha maji cha Mto Simba kilichopo Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, umbali wa kilomita 65 mpaka Longido. Mradi huo utagharimu Sh15.8 bilioni na utahudumia watu 26,145 utakapokamilika Julai, 2018.

Majaliwa alisema Rais John Magufuli aliahidi kwenye kampeni zake za uchaguzi kwamba atapeleka maji kwenye wilaya hiyo na sasa ametimiza.

“Nataka niwahakikishie, mkakati wa kupeleka maji uko kwenye kampeni iliyoanzishwa na Rais wetu ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hii imewezesha ongezeko la fedha za bajeti kwenye wizara yenyewe,” alisema Waziri Mkuu.

Kiongozi huyo alisema lengo la Serikali ni kuongeza pia maji kwa ajili ya kunywesha maji ili mifugo ya wananchi nayo iweze kupata maji sambamba na matumizi mengine ya majumbani.

Alisema bado kuna haja ya kutumia vyanzo vya maji ya mvua ili kuvuna maji hayo kwa ajili ya kujaza mabwawa ya kunyweshea mifugo. Alisema mradi huo ni mkubwa na maji yatakuwa ya uhakika na mengi yatapatikana.

“Namuagiza Waziri wa Maji, endelea kufuatilia vyanzo vingine vya maji, leta wataalamu waje wafuatilie vyanzo vya maji. Ukitoka hapa uende na Loliondo, wataalamu wako watafute vyanzo vya maji ili kumaliza kabisa tatizo la maji,” alisema.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alisema mradi wa maji wa Longido umekuwepo tangu mwaka 2010, lakini Serikali ya Awamu ya Tano imetenga fedha na kuanza kuutekeleza.

Alisema upatikanaji wa maji Longido ni asilimia 15 pekee, kiwango ambacho bado kipo chini ukilinganisha na kiwango cha kitaifa cha upatikanaji wa maji cha kitaifa ambacho ni asilimia 72 huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 85.

“Wananchi nanyi mjenge utamaduni wa kuvuna maji ya mvua wakati ujenzi wa mradi huu unaendelea,” alisema Lwenge na kuwataka wakandarasi watakaojenda mradi huo kufanya kazi kwa viwango vilivyowekwa na kuhakikisha unakamilika kwa wakati.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad