Masharti Mapya yasababisha Maduka ya Fedha za Kigeni Kufungwa

Masharti Mapya yasababisha Maduka ya Fedha za Kigeni Kufungwa
Maduka yapatayo 10 ya kubadilishia fedha yamefungwa, ikiwa ni miezi mitatu kabla ya masharti mapya ya kupata leseni kuanza kutumika,

Kwa takriban wiki tatu, ambazo gazeti la The Citizen limekuwa likifuatilia kwa karibu, maduka hayo yamekuwa hayafanyi shughuli hizo za kubadilisha fedha na watu wa ndani wamedokeza kuwa idadi inaweza kukua hadi kufikia maduka 100 kutokana na kukaribia kwa tarehe ya mwisho kabla ya masharti hayo kuanza kutumika.

Kwa mujibu wa The Citizen, maduka ambayo yamefungwa kwa takriban wiki tatu ni pamoja na Ruby, Maddy, Europa, Money Link, Nana na Tungwe.

Hata hivyo, haikuweza kuthibitisha mara moja kama kufungwa kwa maduka hayo ni moja kwa moja au ni kwa muda na kama ni matokeo ya kuanzishwa kwa masharti hayo mapya ya kupata leseni ya kuendeshea biashara hiyo au la.

Mkurugenzi wa Benki Kuu Tanzania (BoT) anayehusika na usimamizi wa benki, Kennedy Nyoni alisema juzi kuwa maduka yapatayo saba yameitaarifu taasisi hiyo kuu ya kifedha nchini kuwa yanaachana na biashara hiyo ya ubadilishaji fedha, lakini hakuwa tayari kuyataja.

Mmoja wa watu wanaoendesha biashara hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia The Citizen kuwa masharti mapya ya utoaji leseni ni magumu kwa wanaoendesha biashara ya ubadilishaji fedha na kukisia kuwa idadi ya maduka yatakayofungwa inaweza kuongezeka hadi kufikia 100.

“Kusema kweli, baadhi yetu tuko hapa kwa sababu tu bado tuna mikataba na upangaji kwenye majengo tunayoendeshea biashara,” alisema mfanyabiashara huyo.

“Mara tu mkataba utakapoisha, nasi pia tutafunga.”

Alisema sharti kwamba anayetaka leseni ya biashara hiyo ni lazima aweke dhamana ya Sh300 milioni halina uhalisia kwa sababu kipato anachoweza kupata kirahisi ni Sh8 milioni tu katika kipindi cha miezi mitatu kwa kuwekeza kiwango kama hicho cha fedha katika akaunti maalumu ya benki ya biashara.

“Kwa nini mtu apitie mchakato mgumu wa kutafuta Sh300 milioni na baadaye alipe kodi ya pango, na ajira katika kipindi hiki ambacho biashara si nzuri?” alihoji.

“Kwa nini usiweke fedha hizo katika akaunti maalumu ya benki na kupata riba bila ya kutoka jasho?”

Lakini Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu aliiambia The Citizen kuwa masharti hayo hayatabadilishwa.

“Waendeshaji wote wa maduka ya kubadilishia fedha wameshataarifiwa mabadiliko yaliyofanywa katika kiwango cha mtaji kinachotakiwa na wanategemewa kuwa wameyazingatia kabla ya tarehe ya mwisho kufika,” alisema Profesa Ndulu.

BoT ilipitia upya kanuni zinazosimamia uendeshaji wa maduka ya kubadilishia fedha nchini mwezi Juni, ikiwa ni mpango wa kukabiliana na utakatishaji fedha.

Kumekuwa na tuhuma kuwa maduka hayo yamekuwa yakitumiwa na wafanyabiashara na viongozi wa Serikali kutakatisha fedha.

Kutokana na kupitia upya kanuni hizo, BoT ilipandisha kiwango cha mtaji cha uanzishaji maduka hayo, kuzuia utoaji wa leseni kwa maduka mapya na kutaka wanaoendesha biashara hiyo kuomba upya leseni.

“Kiwango kipya cha mtaji kimeongezwa kutoka Sh100 milioni hadi Sh300 milioni kwa maduka ya daraja ‘A’ na kutoka Sh250 milioni hadi Sh1 bilioni kwa maduka ya daraja ‘B’,” BoT ilisema katika mwongozo wake kwa maduka hayo uliotolewa Juni 21.

Agosti 28, BoT iliongeza muda kwa waendeshaji maduka hayo kutekeleza maagizo hayo kuanzia Septemba hadi Desemba.

“Hii ni kuwajulisha waendeshaji wote wa madula ya kubadilishia fedha kwamba BoT imeongeza muda wa kuomba upya leseni hadi Desemba 31, 2017,” unasema mwongozo huo wa benki hiyo.

Pia, ulitaka waendeshaji biashara hiyo kuhakikisha wanazingatia kiwango cha chini cha mshahara.

Kwa mujibu wa BoT, theluthi mbili ya mtaji huo inatakiwa iwe fedha taslimu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad