Maskini..Kumbe Manji Amenyang’anywa Udiwani kwa Makosa ya Mwaka 2016
0
September 15, 2017
Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo amesema aliyekuwa Diwani wa Mbagala Kuu (CCM), Yusuf Manji alivuliwa cheo hicho kwa kosa la kutohudhuria vikao sita vya mwaka 2016 bila kutoa taarifa.
Manji aliyekumbwa na mikosi ya kesi tangu mwaka huu uanze juzi aliachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam akiwa na wenzake watatu waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kukutwa wakiwa na mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) zenye thamani ya Sh 192.5 milioni.
Kesi hiyo imefutwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) kusema hana nia ya kuendelea nayo.
Mbali na kesi hiyo, Manji pia anakabiliwa na kesi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin aliyosomewa Februari 17, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Septemba 6, Meya Chaurembo aliwaambiwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa walimwondoa kwenye nafasi ya udiwani kwa kukosa sifa ikiwa pamoja na kutohudhuria mikutano sita ya Baraza na Kamati za Madiwani.
Hata hivyo, Manji alishaeleza kuhusiana na kutokubaliana na hatua ya kumvua udiwani na mara baada ya kuachiwa huru, aliulizia kuhusu malalamiko yake aliyowasilisha mahakamani hapo kuhusu udiwani wake yako vipiu lakini Hakimu Shaidi alimueleza kwa kuwa yuko huru ataenda kulishughulikia hilo.
Akizungumza jana kwa njia ya simu na gazeti hili, Chaurembo alisema makosa ya Manji yalitendeka mwaka 2016 kabla hata mikosi ya kukamatwa na kufunguliwa kesi haijaanza.
Mwananchi
Tags