MBUNGE wa Geita Vijijini (CCM), Josephat Kasheku Musukuma, anajiandaa kuanika siri za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Lotson Mponjoli baada ya kushindwa kutimiza sharti lake la kumwomba radhi kutokana na madai ya kumdhalilisha.
Akizungumza na Nipashe jana, Musukuma alisema baada ya muda aliokuwa ametoa kwa kamanda huyo kuomba radhi kupita, ataweka hadharani madudu yote yanayofanywa na RPC huyo wiki ijayo atakapokuwa amerejea mkoani humo akitokea Zanzibar aliko kwa sasa.
"Niko Zanzibar naumwa na kwa leo (jana) sitaweza kulizungumza kwa kina hilo suala," alisema Musukuma ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita na ambaye alikaa mahabusu kwa siku tatu kabla ya kufikishwa mahakamani Septemba 19.
Msukuma na wenzake nane wanakabiliwa na mashtaka manne ya jinai, likiwamo la kula njama.
"Nikirudi (Geita) tu nitaitisha mkutano na waandishi wa habari na kuweka hadharani yale niliyokuwa nimeyaahidi nilipozungumza wiki iliyopita."
Wiki iliyopita, Musukuma alimpa siku nne Mponjoli kumwomba radhi la sivyo ataweka hadharani alizodai kashfa zake, ikiwamo madai ya kujilimbikizia mali.
Musukuma alilalamikia hatua ya RPC huyo kumkamata katika mazingira aliyoita ya kumdhalilisha kwa kumshika suruali nyuma kama mhalifu, wakati yeye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Geita na mwakilishi wa wananchi.
Alisema RPC huyo asipoomba radhi ataanika hadharani alichoita maovu yake, ili vyombo vya uchunguzi kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), vianze kuchunguza.
Musukuma alimlaumu Kamanda huyo kwa kumkamata na kumweka mahabusu wakati angeweza kumwita na kuzungumza naye kwa staha kwa kuwa yeye ni kiongozi wa chama na mwakilishi wa wananchi.
"Tangu CCM iundwe mwaka 1977 mimi nimeweka rekodi ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza kuwekwa ndani na RPC wangu," alisema zaidi Musukuma na kulalamika zaidi:
"Nakwambia RPC kwa kuwa umenichokoza, na kwa kuwa umeamua kuingia kwenye hii ligi, basi jiandae. Umeliamsha dude na mimi nitaliamsha kwelikweli." Alisema kama Mponjoli anataka amani atafute wazee wanaomheshimu kama Mwenyekiti wa CCM na kwenda kuzungumza.
Aliwataka wakazi wa Geita kukaa mkao wa kusikiliza sababu za yeye kukamatwa na RPC huyo na kwamba vitu vyote ambavyo RPC huyo amewekeza mkoa wa Geita na mengine angetaja baada ya siku hizo. Amekuwa kimya hata hivyo.
Alipotafutwa kwa njia ya simu kupata maoni yake juu ya kauli hiyo ya Musukuma jana, Kamanda Mponjoli alisema yeye anazungumzia masuala ya jinai tu.
"Mkiniuliza mambo ya uhalifu nitawaambia, lakini hayo mambo anayosema Mbunge siwezi kuyazungumzia," alisema RPC Mponjoli.
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita ilidaiwa washtakiwa, kwa pamoja, Septemba 13, mwaka huu, majira ya saa nne asubuhi katika ukumbi wa Gedeco unaomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Geita, walipanga njama ya kuweka mkusanyiko usiokuwa na kibali, kuharibu mali na kuweka vizuizi katika barabara ya kuingia Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM).
Mbali na Musukuma ambaye pia ni Mbunge wa Geita, washtakiwa wengine ni Steven Werema (mkulima), Costantine Molandi, Winifrida Malunde, Ngundugu Joseph, Martine Kwilasa, Khadija Said, Maiko Kapaya na Maimuna Mengisi (wote madiwani).
Shtaka la pili Mwasinga alisema linawahusisha watuhumiwa nane kati ya tisa, ambapo alidai kwamba Septemba 14, majira ya saa 12 asubuhi katika kijiji cha Mtakuja, walifanya mkusanyiko usio halali.
Mwasinga alisema kuwa katika shtaka la tatu, Septemba 14, majira ya saa 12 asubuhi, washtakiwa hao nane walitenda kosa la kufunga barabara ya kuingia na kutoka GGM na kusababisha wafanyakazi wa mgodi na watu wengine kushindwa kutumia barabara hiyo.
Katika shtaka la nne, Mwasinga alidai mahakamani hapo kuwa Septemba 14, majira ya saa 12 asubuhi, washtakiwa hao nane kwa pamoja walitenda kosa la kuharibu bomba la maji katika kijiji cha Nungwe linalosafirisha maji kwenda GGM, hali iliyosababisha hasara ya Sh. milioni 12.25 na kupungua kwa huduma ya maji katika mgodi huo na kwa wananchi wa mji wa Geita.
Washtakiwa wote tisa kwa pamoja walikana mashtaka hayo huku mwendesha mashtaka wa serikali akiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa madai upelelezi haujakamilika.
Akiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ushindi Swalo alisema dhamana kwa washtakiwa hao iko wazi na kila mmoja alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh. milioni tano.
Washtakiwa walitimiza masharti ya dhamana na wote wako nje. Washtakiwa wanatetewa na mawakili Neema Christian na Deo Magengeli.
Nipashe
Mbunge Msukuma Kuanika Siri za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita
0
September 29, 2017
Tags