Mchungaji Afungwa Miaka 30 Jela kwa Kubaka Muumini Wake

Mchungaji Afungwa Miaka 30 Jela kwa Kubaka Muumini Wake
MCHUNGAJI wa kanisa la kilokole la Victoria lililopo Sokoni One jijini Arusha, Chrisantus Mboya (35), amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka muumini wake wa chini ya miaka 16.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Arusha, Nestori Ballo, alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Juni 3, mwaka huu na mahakama imeridhika na mashahidi sita waliotoa ushahidi.

Hakimu Ballo alisema katika hukumu yake kuwa, muathirika (jina tunalihifadhi), aliieleza mahakama jinsi alivyobakwa na mchungaji huyo nyumbani kwake na mahakama kujiridhisha mchungaji huyo kutenda kosa hilo.

Alisema daktari wa hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ambaye alikuwa shahidi wa nne katika kesi hiyo, aliieleza mahakama kuwa muathirika hakukutwa na majeruhi sehemu ya siri, lakini aliingiliwa bila ya ridhaa yake.

Hakimu Ballo alisema, shahidi wa pili ambaye ni dada wa muathirika, alidai mahakamani hapo kuwa mchungaji aliwaambia kuwa muathirika alikuwa na pepo hivyo alipaswa kuombewa na maombi hayo yanapaswa kuwa maalumu nyakati za usiku kwa ajili ya afya yake.

Alisema shahidi huyo alikubaliana na ushauri wa mchungaji na muathirika aliambiwa na kupelekwa mapema kanisani kwa ajili ya maombi hayo, lakini hilo halikufanyika na badala yake alimpeleka nyumbani kwake na kumvutia chumbani na kuanza kumbaka.

Baada ya mahakama kumtia hatiani mchungaji Mboya, Hakimu Ballo alimpa nafasi Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Rose Sulle, kutoa maoni yake ambaye alitaka adhabu kali itolewe kwa mchungaji huyo ili iwe fundisho kwa wengine wenye kukiuka maadili ya kiimani.

Sulle alisema jamii ina imani na wachungaji kuwa ni watu wenye maadili.

Alisema adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa wachungaji wengine wanaotumia mwanya kwa waumini kuwa na
matatizo ya kiafya kufanya vitendo viovu vya kubaka.

Aidha, mchungaji huyo alipopewa nafasi ya kujitetea, aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana familia.
Hata hivyo, utetezi huo haukumsaidia na kupewa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela.

Aidha, aliambiwa kama hajaridhika na hukumu hiyo anaweza kukata rufaa mahakama kuu kupinga
hukumu hiyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad