Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema litaanza kuwashtaki watakaovunja uhuru wa Habari ikiwamo kuwazuia waandishi wa Habari kupata taarifa, vipigo na matukio yote ya udhalilishaji dhidi yao.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa MCT, Ofisa Miradi wa Baraza hilo Pili Mtambalike amesema matukio hayo yanaongeza hofu na kuwafanya waandishi washindwe kutimiza wajibu wao kikamilifu.
Mtambalike amesema pamoja na hatua nyingine wataanza kuwachukulia hatua ikiwamo kuwashtaki wale watakaofanya hivyo huku akiwaasa wanahabari kutoa taarifa vinapotokea vitendo vinavyokiuka uhuru wa habari.
"Tukio likitokea tutalichunguza na tukijiridhisha na tukio linaweza kupelekwa mahakamani tutashtaki," amesema.
Hata hivyo amesema kwa mwaka huu zaidi ya matukio 11 yameripotiwa ikiwamo lile la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kuvamia kituo cha TV cha Clouds.
Rais wa MCT, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo amesema baraza hilo lilianzisha Rejista ya Matukio ya Uvunjaji Haki wa Habari (PFVR) ili kuhakikisha kila tukio linaripotiwa na kuchukuliwa hatua.
Amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na takwimu sahihi za matukio hayo ili wanapowasiliana na Serikali kuwe na mfano halisi.