MEYA wa Ubungo, Boniface Jacob (Chadema), amehojiwa kwa saa tatu na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwa madai ya kutumia ofisi za umma kufanya vikao vya chama.
Akizungumza baada ya kumaliza kuhojiwa jana jijini Dar es Salaam, Jacob alisema, alitoa utetezi wake kuwa hakufanya kikao isipokuwa alitembelewa na wageni wa chama, lakini kama wanaona anastahili kuwajibishwa wafanye hivyo.
Kadhalika Jacob alisema alitoa ushaidi wa matumizi mabaya ya ofisi za umma, yanayofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nimewaeleza Sekretarieti kuwa, pia CCM, kimekuwa kikifanya vikao vyake Ofisi za Ikulu na wamenieleza hakuna aliyewahi kulalamika. Hivyo nimelazimika kuandika barua ya malalamiko juu ya kitendo hicho,” alisema.
Kuitwa na kuhojiwa kwa Jacob na Sekretarieti hiyo kumetokana na kitendo chake cha kumkaribisha ofisini kwake Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani.