Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata watu wawili akiwamo mlinzi wa Suma JKT na mfanyakazi wa NBC, Tawi la Tangibovu wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kujeruhiwa kwa risasi, meja jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Vincent Mritaba.
Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema jana kuwa Septemba 11, saa 11 jioni maeneo ya Tegeta Masaiti, jeshi hilo lilipata taarifa ya Mritaba kuvamiwa na watu wawili wasiojulikana ambao walimjeruhi kwa risasi begani, tumboni na mkononi na kumpora Sh5 milioni.
Alisema tukio hilo lilitokea baada ya mstaafu huyo kutoka kuchukua fedha hizo katika benki hiyo tawi la Tangibovu akiwa kwenye gari lake.
Mambosasa alisema alipofika nyumbani kwake alipiga honi na alifunguliwa geti na mlinzi wake, Godfrey Gasper.
Alisema geti lilipofunguliwa ghafla pikipiki iliyokuwa na watu wawili ilisimama na kulifuata gari huku wakiwa na silaha aina ya bastola. Watu hao walishambulia upande wa kulia wa dereva na kioo cha mbele.
Mambosasa alisema cha kushangaza wakati mlinzi huyo anaenda kufungua geti silaha yake aina ya shotgun yenye namba TZCAR9644, aliiacha chini ya kitanda ndani ya kibanda chake cha ulinzi.
Alisema wakati wa tukio watuhumiwa walimwambia akimbie katika eneo hilo na yeye alitii amri hiyo, jambo ambalo linatia shaka.
“Ninavyojua askari wa Suma JKT anapewa mafunzo ya ukakamavu haiwezekani uache silaha chini ya kitanda unakwenda kufungua geti kitu ambacho sikubaliani nacho,”alisema.
Alisema walipofuatilia mawasiliano ya mmoja wa wahudumu wa benki hiyo walibaini alikuwa anapanga mipango na watu mbalimbali wanaokwenda katika benki hiyo. Alisema msako mkali unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika katika tukio hilo.
Pia, alisema wanaendelea kuwasaka watu waliohusika na uhalifu kwenye ofisi ya mawakili ya Prime Attorneys na watakapokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Wakati huohuo, Kamanda Mambosasa alisema wamemuua mtu anayetuhumiwa kwa ujambazi, Anaf Kapela ambaye alishiriki katika matukio mbalimbali likiwamo la mauaji ya askari nane na kupora silaha saba katika tukio la Mkengeni Kibiti mwaka huu.
Mambosasa alisema matukio aliyoshiriki mtuhumiwa huyo ni mauaji ya mkuu wa upelelezi Wilaya ya Newala 2013, uvamizi wa Kituo cha Polisi cha Stakishari jijini Dar es Salaam 2015, kuua askari watatu na kupora silaha mbili aina ya SMG katika Benki ya CRDB eneo la Mbande, Benki ya Access iliyopo Mbagala, Benki ya NMB iliyopo Mkuranga na uhalifu mwingine uliotokea 2016.