Uongozi wa Kampuni ya Williamson Diamonds Limited (WDL) umesitisha kwa muda baadhi ya shughuli za uzalishaji katika mgodi huo.
Taarifa ya uongozi wa mgodi huo kwa wafanyakazi jana, zilisema huduma za uzalishaji zimesimamishwa isipokuwa huduma maalumu za ulinzi, tiba, umeme, maji, zimamoto na usafiri unaohitajika katika huduma hizo.
Taarifa hiyo ilisema huduma za utawala zitaendelea kufanya kazi wakati huduma nyingine zitakazoendelea kuendeshwa na mgodi itatolewa taarifa uzalishaji utakaporejea.
Taarifa hiyo ilisema Kampuni ya WDL inasubiri agizo la kuacha kusafirisha nje almasi yake kutoka mgodini, kifurushi namba W1-FY18.
Hata hivyo, taarifa za ndani zinasema Serikali imezuia kusafirisha kifurushi hicho kwa misingi ambayo haijawasilishwa rasmi kwao licha ya kuona taarifa hizo kupitia vyombo vya habari.
“Hatuwezi kutoa maoni yoyote kutokana na matokeo ya uchunguzi huo.
“Vifurushi vyote vinavyosafirishwa kwa biashara nje hukadiriwa thamani yake hapa mgodini na watumishi wa ‘TANSORT’ ambacho ni kitengo cha kukadiria thamani ya almasi na vito wanaowawakilisha Wizara ya Nishati na Madini.
“Kifurushi kinavyosafirishwa kinapigwa mihuri miwili ya vyombo viwili vya Serikali, sisi uongozi hatuna ujuzi wanaoutumia ‘TANSORT’ wa kukadiria kwa muda malipo ya mrabaha kwa Serikali.
“Yanakamilishwa baada ya kupatiwa matokeo halisi ya zabuni ya wazi ya almasi za WDL na uaminifu wake unathibitishwa na TANSORT kutoka wizarani,’’ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kamishna wa Nishati na Madini, Benjamin Mchwampaka jana alisema taarifa ya mgodi huo haijafika kwake bali ameiona kwenye mitandao ya jamii.
Alisema mpaka sasa hawezi kujua athari za kusimamisha uzalishaji wa mgodi huo hadi atakapopata taarifa rasmi kutoka kwa uongozi.
“Nimeziona mitandaoni, sijapata taarifa kutoka kwao wenyewe itabidi kuitafakari ikifika kesho (leo).
“Lazima niweze kujua hilo na niweze kufahamu pia athari na wamefunga maeneo gani na athari hata kwa wafanyakazi itakuwa kwa kiasi gani ,’’alisema Mchwampaka.
Hivi karibuni wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), walikamata mzigo wenye madini ya almasi yenye uzito wa kilo 29, dakika tano kabla ya ndege kupaa, huku yakiwa yameandikwa yana kilo 14.3.
Inaelezwa walioshiriki kufanya udanganyifu huo ni watumishi wa serikali waliopewa dhamana ya ukaguzi na uthaminishaji katika mchakato wa kuanzia mgodini hadi kuidhinisha usafirishaji wa madini hayo nje ya nchi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango, juzi alitembelea uwanja wa JNIA kwa ajili ya kutoa maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka (DPP), Mganga Biswalo.
Alisema Tanzania imepigwa vya kutosha hivyo wote waliohusika katika udanganyifu huo washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Waziri alisema wafanyakazi wote waliohusika kuanzia hatua ya uchimbaji wa madini hayo mpaka kule yanakosafirishwa, wamulikwe na vyombo vya dola kubaini uhalali wa mali zao wanazomiliki.
Ilielezwa kuwa wamiliki wa mgodi wa madini hayo walisema yana thamani ya Dola za Marekani milioni 14.8, lakini baada ya uchunguzi ilibainika thamani yake ni Dola za Marekani milioni 29.7.