Mgogoro Kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita na Madiwani Ngoma Ngumu
0
September 19, 2017
Mgogoro kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na baraza la madiwani wa halmashauri mbili za Geita umechukua sura mpya, baada ya kikao cha kutafuta suluhu kukwama kutokana na mahudhurio hafifu.
Septemba 14, uongozi wa Mkoa wa Geita uliwataka madiwani waliofunga barabara za kuingia GGM kuwa watulivu kusubiri kikao na kamishna wa madini.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi alisema wamekubaliana kuahirisha kikao hicho hadi madiwani wanaoshikiliwa polisi watakapofikishwa mahakamani na kupata dhamana, ndipo waitishe kikao maalumu atakachoshiriki pia kamishna wa madini nchini.
Madiwani 10 akiwamo Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma wanashikiliwa na polisi wakiwemo wananchi watano na Katibu wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya Geita, Ally Rajabu.
Kushikiliwa kwao kunatokana na vurugu zilizotokea Alhamisi iliyopita kwa madiwani kudaiwa kufunga barabara zinazoingia GGM wakishinikiza kulipwa Dola 12 milioni za Marekani (zaidi ya Sh26 bilioni zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.
Kamishna wa madini nchini, Benjamin Mchwampaka jana alisema baada ya kumalizika kikao kilichohudhuriwa na kamati za ulinzi na usalama za mkoa na wilaya na ofisi ya madini ya mkoa kuwa hawakuendelea na kikao kingine kutokana na madiwani kutohudhuria.
Mchwampaka alisema lengo la kufika Geita ni kutafuta muafaka baina ya pande hizo lakini imeshindikana kutokana na baadhi ya madiwani kushikiliwa na vyombo vya dola na wengine kutohudhuria kikao hicho.
Madiwani hao wanasema fedha wanazoidai GGM ni haki yao kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mgodi ulipaswa kulipa ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 lakini hawakulipa na badala yake walilipa Dola 200,000 kwa mwaka tangu 2004 hadi 2013 kinyume cha sheria.
Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Jamii wa GGM, Manase Ndoroma alisema kinachosababisha mgogoro kati ya pande hizo ni kupingana kwa sheria ambazo zote zimetungwa na Bunge.
Alisema sheria ya madini iliwaruhusu kulipa Dola 200,000 kwa mwaka, huku sheria ya baraza la madiwani ikiwa imepitisha malipo ya asilimia 0.3 jambo linalosababisha mgogoro na suluhisho pekee ni kwenda mahakamani.
Tags