Miili ya watoto watatu waliofariki dunia kwa mlipuko wa bomu kwenye eneo la mazoezi ya kijeshi wilayani Monduli imeagwa na kusafirishwa kwa maziko katika Kijiji cha Nafco.
Shughuli ya kuaga miili hiyo imefanyika leo Jumatatu katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli.
Watoto hao walifariki dunia Ijumaa jioni katika Kijiji cha Nafco kilichopo Kata ya Loksale walipokuwa wakichunga ng'ombe.
Ilielezwa watoto hao walilipukiwa na bomu walipokuwa wakilichezea wakidhani ni mpira.
Watoto waliofariki dunia wametajwa kuwa ni Johnson Daniel, Lendisi Saitabau na Samweli Nyangusi.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Idd Kimanta ameongoza kamati ya ulinzi na usalama kuaga miili ya watoto hao.