Mke wa mwigizaji nguli, Said Ngamba ‘Mzee Small’, Fatuma Said amesema yupo kwenye kipindi kigumu cha maisha kutokana na upweke alionao na kwa sababu marafiki wa marehemu mumewe wamemtenga si kwa salamu wala barua.
Akizungumza kwa uchungu na mwanahabari wetu nyumbani kwake Tabata-Kimanga jijini Dar, mama Small alisema tangu mumewe afariki ni miaka mitatu sasa, lakini mara kwa mara amekuwa akimkumbuka na kuishia kulia.
Alisema kwa sasa anapambana mwenyewe kimaisha bila ubavu wake hivyo kujikuta akipata ugumu wa maisha.
“Kwa kweli nina maisha magumu japo namshukuru Mungu niko mzima wa afya, sina kazi ninayoitegemea zaidi ya biashara yangu ya kuuza chapati kwani hata ule mradi wa maji tuliokuwa nao kabla mume wangu hajafariki, sasa ni kama haupo.
“Haupo kwa sababu serikali imejitahidi kuweka mabomba ya maji baridi, hivyo watu hawawezi kununua maji ya chumvi labda itokee maji yamekatika, hayatoki.
“Pia nategemea hela za wapangaji lakini hivyo sio nyingi zinasaidia kumsomesha mtoto shule tu.
“Kama unavyojua sasa hivi hali ya uchumi ni ngumu. Kila kitu ni ghali, nadunduliza hivi katika chapati lakini fedha zote unajikuta umezitumia kwenye mahitaji mengine.
“Mwanaume ni mwanaume tu. Alipokuwepo mume wangu nilikuwa sipati maumivu haya kwani angalau yeye alikuwa na wadau wake wa sanaa ambao walikuwa wakimpa fedha za kutufanya tuishi vizuri.
“Kwa sasa kama unavyoona hapa naishi mwenyewe na wanangu watatu alioniachia na mmoja wake niliyemlea, shughuli zao za kubangaiza tu, kama huyo mwingine alitamani awe msanii lakini hakupata wa
kumshika mkono,” alisema mama Small.
Akiendelea kuzungumzia maisha yake ya sasa, mama huyo alisema pamoja na yote, anajivunia kuona anapo mahali pa kuishi kwani marehemu aliacha nyumba mbili na familia ya mumewe yuko nayo vizuri bila tatizo.
“Sina tatizo na yeyote yule na wala sina mwanaume wa kuziba pengo lake tangu aondoke mume wangu, ila akitokea wa kunioa nitakubali, kinachoniumiza sana ni wasanii wenzake kunitupa mfano Tupatupa alikuwa kama pacha wake lakini hata watoto hawajulii hali,” alisema mama Small.
Mke wa Mzee Small Atengwa Asimulia Magumu Anayopitia Toka Mumewe Afariki
0
September 29, 2017
Tags