Mkuu wa Majeshi Atoa Tahadhari kwa Wananchi


Mkuu wa Majeshi Atoa Tahadhari kwa Wananchi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo ametoa tahadhari kwa wananchi kwamba kuna matapeli wanaojifanya wanaajiri vijana kujiunga na jeshi.

Amesema watu hao wanadai fedha ili kuwasajili vijana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jambo ambalo ni kinyume na taratibu za jeshi kuajiri vijana kwa JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Mabeyo ameonya kwamba mtu yeyote atakayetapeliwa na watu hao basi naye atahesabika kama mmoja wa watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kuchukuliwa hatua mara moja.

"Maongezi ya mtu na mtu hatuyatambui, ukitapeliwa nyamaza kimya kwa sababu ukilalamika kwetu na wewe utachukuliwa kama sehemu ya watoa rushwa," amesema Jenerali Mabeyo.

 Mkuu huyo wa majeshi amebainisha njia mbalimbali ambazo wanazitumia kuajiri vijana jeshini kuwa ni kuwachukua wale waliopitia mafunzo ya JKT au pale wanapotaka watu wenye taaluma adimu kama vile madaktari, wahandisi au wanasheria.

Amebainisha kwamba jeshi linapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wanachukua hatua kila wanapopata taarifa ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wahusika na kuwakamata.

 "Kuna mmoja alikusanya vijana 15 na kila kijana akatakiwa kulipa Sh1 milioni. Aliwapangia chumba sehemu kisha akatoweka," amesema Mabeyo na kusisitiza kuwa wengi wanaofanya vitendo hivyo ni raia, wanajeshi ni wachache na wanachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja.

Kuhusu matukio ya watu kupigwa risasi, CDF amesema wakati wote yanapotokea matukio hayo, vyombo vya ulinzi na usalama vinakabiliana nayo mara moja na hali inakuwa shwari.

 "Kwa ujumla hali iko shwari, huwezi kusema Tanzania siyo salama kwa sababu ya matukio mawili ya kijambazi. Mambo tunayotaka kujiridhisha nayo kwa sasa ni wapi wanapata silaha na wanatoka wapi," amesema Mabeyo.

       
 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad