Unywaji wa pombe za kienyeji ambao wakati mwingine huambatana na baadhi ya wanywaji kufanya vurugu, ukatili wa kijinsia, uporaji na hata kujeruhi umemsukuma mkuu wa wilaya kuagiza itungwe sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga ameziagiza halmashauri mbili zilizopo wilayani humo zitunge sheria ndogo za udhibiti wa kutengeneza, kuuzaji na kunywa pombe hizo ili kukomesha matukio ya aina hiyo yanayotokea kila mara.
Mofuga alitoa agizo hilo juzi kwenye mkutano na wananchi uliolenga kukomesha matukio ya kikatili yanayosababishwa na unywaji wa pombe za kienyeji.
Alisema yapo matukio mengi ya kikatili yanayotokea sehemu tofauti katika eneo hilo yanayosababishwa na pombe za kienyeji, hivyo suluhisho ni utungwaji wa sheria ndogo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema endapo halmashauri ya mji na ile ya wilaya zikitunga sheria ndogo, maeneo yaliyokithiri kwa pombe za kienyeji katika kata za Dongobesh na Sanu yatamalizika.
Alisema japo kuna sheria mama inayoongozwa na Katiba, kutungwa kwa sheria hizo kutapunguza matukio hayo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya wilaya hiyo, Melkiore Miniko alisema pia utungwaji wa sheria hizo utapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya kifamilia.
Miniko alisema matukio ya kikatili yanasababisha na pombe haramu ya gongo na zingine za kienyeji zinazochangia kurudisha nyuma maendeleo.
Alisema wamekuwa wakipokea malalamiko mengi ya ukatili kwa watoto na kutelekezwa familia kunakotokana na wazazi wengi kujiingiza kwenye unywaji wa pombe haramu, hivyo suluhisho ni kuwapo na sheria ndogo. Ofisa huyo alisema kuwa licha ya kuwapo kwa sheria ya leseni ya vileo, inapaswa kuongezwa sheria ndogo ili kupunguza madhara hayo kwa jamii.