Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi amepiga marufuku ubomoaji wa nyumba bila idhini yake.
Pia, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata madalali wa Mahakama wanaotumiwa kubomoa nyumba za wananchi bila kupata kibali kutoka kwake.
Amesema hayo leo Jumatano, alipozungumza na wananchi wa Kata ya Kunduchi alipotembelea eneo hilo akiwa ziarani kikazi kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Soko la Samaki.
Marufuku hiyo imetolewa baada ya Diwani wa Kunduchi, Michael Urio kutoa kero kwamba kuna watu wamevunjiwa nyumba pasipo viongozi wa maeneo husika kushirikishwa.
Hapi amesema kumekuwa na kesi nyingi ofisini kwake kuhusu kubomolewa nyumba na watu aliowaita matapeli na kwamba, kuanzia sasa hakuna atakayebomoa bila ya yeye kujua.
Amesema lengo ni kuhakikisha nyumba zinazobomolewa zimeainishwa na Mahakama kwa kuwa madalali wengine wanaghushi hukumu.
"Ni marufuku mtu kuvunja nyumba bila mimi na vyombo vyangu kuwa na taarifa. Hatuwezi kuvumilia huu mchezo, kama kuna dalali amekwenda kuvunja nyumba ambayo haijaainishwa kwenye hukumu ya Mahakama akamatwe mara moja," amesema.
Hapi amesema, "Zipo kesi zimetokea kwenye wilaya yetu, wale madalali wamekuwa wakivunja nyumba ambazo hazijaainishwa, Mahakama inasema nyumba namba 13 wao wanavunja nyumba namba 23," amesema.