JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili akiwemo mlinzi wa makaburi ya Wangazija yaliyopo Upanga, Mohamed Maganga (61) wakiwa na bunduki mbili aina ya Uzigun na Riffle, bomu la kurusha kwa mkono na risasi 167.
Mbali na Maganga ambaye ni mkazi wa Pugu, mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa ni Rahma Almas maarufu Baby (37) ambaye alikiri kuhifadhi silaha hizo zilizotumika katika matukio mbalimbali ya uhalifu, ikiwemo mauaji ya Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la PALMS Foundation, Wayne Lotter (52).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 16, mwaka huu saa 11:50 jioni, maeneo ya makaburi ya Wangazija yaliyopo Upanga.
“Mtuhumiwa huyo (Baby) aliwaelekeza askari kuwa silaha hizo amezificha katika makaburi hayo, ndipo askari walifika eneo la tukio na mtuhumiwa ambapo walizikuta silaha hizo mbili moja ikiwa ni aina ya Uzigun na Riffle ambayo imekatwa mtutu na kitako chake na namba zikiwa zimefutwa zote huku zikiwa zimefukiwa kwenye shimo,” alifafanua Kamanda Mambosasa.
Alisema Maganga alisaidia kuchimba shimo na kuzilinda silaha hizo na katika mahojiano, alikiri silaha hizo zililetwa na Rahma, lakini hakutoa taarifa hadi alipokamatwa. Alisisitiza kuwa watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo linawashikilia watu watano wanaotuhumiwa kuvunja ofisi za Kampuni ya Mawakili ya Prime Attorneys inayomilikiwa na mmoja wa mawakili wa mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji, Hudson Ndusyepo.
Kamishna Mambosasa alisema Septemba 12, mwaka huu walipokea taarifa za kuvunjwa kwa ofisi za mawakili hao na kuibwa kasiki iliyokuwa na fedha taslimu Sh milioni 3.7, kompyuta mpakato na nyaraka mbalimbali za wateja wao.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa ni Said Salehe (47) mkazi wa Mbezi Louis, Mustapha Said (35) mkazi wa Magomeni Mwembechai, Somfi Somfi (52) mkazi Magomeni Mapipa, Iman Mhina (36) mkazi wa Kimara Mwisho na Hussein Suleiman (45) mkazi wa Kigogo Mbuyuni.
“Katika mwendelezo wa tukio hilo watuhumiwa watano wamekamatwa baada ya operesheni kali ya kuwatafuta waliovunja ofisi hiyo ya Prime Attorneys ambao wamekamatwa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam,” alieleza.
Alifafanua kuwa baada ya mahojiano watuhumiwa hao walikiri kushiriki tukio hilo na kuonesha kasiki la fedha pamoja na mitungi mitatu ya gesi iliyotumika kukatia kasiki hilo. Kwa mujibu wa kamanda huyo, watuhumiwa hao walienda Magomeni Mapipa, Mtaa wa Dosi kwa mtuhumiwa aitwaye Somfi na baada ya kulifungua na kukuta hakuna fedha, walilichukua na kulitelekeza eneo la Kigogo daraja la Madaba.
Alisema upelelezi unaendelea ili kuwabaini watumiwa wengine walioshiriki katika tukio hilo. Wakati huo huo, watuhumiwa watatu wa ujambazi akiwamo anayejulikana kwa jina la Shafi aliyetoka gerezani hivi karibuni kwa rufaa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, wamefariki dunia kutokana na majibizano ya risasi walipokwenda kufanya uhalifu kwenye ghala lililopo maeneo ya Tazara.
Mtuhumiwa mwingine anayejulikana kwa jina la Babu Jaffari ambaye ana matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, ambaye kwa mara ya mwisho alikuwa akiripoti Kituo cha Polisi Chang’ombe na mtuhumiwa Mbegu maarufu kama Malon ambaye anatafuta kazi za kupora.
“Majambazi hao walifariki wakati wanapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu baada ya kuvuja damu nyingi na msako mkali unaendelea kumsaka jambazi aliyetoroka na gari waliotumia majambazi hao,” alieleza.
Akielezea tukio hilo, alisema Septemba 15, mwaka huu, saa 11:20 jioni maeneo ya Vingunguti- BECCO Mkoa wa Kipolisi Ilala, askari wa kikosi cha kupambana na ujambazi walipata taarifa kuwa kuna majambazi wanakwenda kufanya tukio la kiuhalifu kwenye moja ya maghala yaliyopo maeneo la Tazara.
Aidha, alisema askari waliweka mtego na kulisimamisha gari aina ya Toyota Mark II rangi ya blue, ambalo namba zake za usajili hazikufahamika na baada ya kugundua kuwa askari wanawafuatilia majambazi hao, walianza kuwashambulia askari kwa risasi ndipo askari wakajibu mashambulizi na kuwajeruhi.
Alisema eneo la tukio palikutwa bastola moja aina ya Browning yenye risasi tatu moja, ikiwa chemba tayari kwa kutoka maganda matatu ya risasi zilizofyatuliwa kutoka katika bastola ya majambazi.