Leo timu ya wachunguzi iliyoundwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kikosi cha kupambana na rushwa ilifanya kikao cha kuanza uchunguzi mpana pamoja na mwenendo wa Msajili wa Mahakama ya Juu, Esther Nyaiyaki.
Hatua hiyo imekuja baada ya mpiga kura Rashid Mohammed kuwasilisha malalamiko Ijumaa iliyopita kupitia kwa mwanasheria wake Kioko Kilukum akidai ripoti ya uchunguzi wa matokeo ya uchaguzi au fomu zake ilighushiwa.
Mohammed alidai kwamba ripoti ya uchunguzi iliyotumiwa na majaji wengi katika hukumu yao dhidi ya matokeo ya urais yanayobishaniwa ilikuwa na ugunduzi tofauti na nyaraka zilizotumiwa na Jaji Njoki Ndung'u.
Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa (EACC) ilisema timu hiyo iliundwa mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mohammed.
Mwishoni mwa wiki DPP, Keriako Tobiko aliviagiza vyombo vya dola kuanzisha uchunguzi dhidi ya maofisa wa juu wa IEBC kuangalia ushiriki wao katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 ambao matokeo yake yalifutwa na Mahakama ya Juu Septemba Mosi.
Tobiko amewapa siku 21 DCI Ndegwa Muhoro na yule wa EACC, Halakhe Waqo kumkabidhi matokeo ya uchunguzi wao.
“Kwa hiyo ninakuandikia kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 157 (4) ya Katiba na Sheria ya Makosa ya Uchaguzi 2017 ili kukutaka ufanye uchunguzi wa pamoja, wa kina na wa haraka katika makosa na uhalali ulioonekana na Mahakama Kuu kufanywa na IEBC katika uchaguzi wa rais kwa lengo la kuamua ikiwa uchaguzi ulikuwa na makosa mengine ya jinai yanayoweza kuwa yalisababishwa na maofisa wa IEBC,” alisema Tobito.
Agizo hilo la DPP limekuja wakati IEBC ilitarajiwa leo kutoa jibu kuhusiana na masharti yaliyotolewa na muungano wa Nasa unaotaka uwapo mkutano baina ya pande zinazoshiriki kabla ya uchaguzi wa marudio uliopangwa kurudiwa Oktoba 26.
Uamuzi huo kwa namna yoyote usipotekelezwa unaweza kuathiri mwenendo wa mchakato wa uchaguzi huo katika mazingira yanayoonyesha kwamba ndani ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka ‘kunawaka moto’, kutokana na maofisa wake wa ngazi za juu kutakiwa na Nasa wajiuzulu kwa kuboronga uchaguzi huo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa EACC Halakhe Waqo alisema timu yao na ile kutoka DCI itafanya kazi pamoja kwa vile suala linalochunguzwa linafahamika.