Msigwa Afunguka Namna Wakenya Wanavyoshangaa Hadhi za Wabunge wa Tanzania

Msigwa Afunguka Namna Wakenya Wanavyoshangaa Hadhi za Wabunge wa Tanzania
Tangu mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliposhambuliwa kwa risasi akiwa mjini Dodoma Septemba 7, kumekuwa na malumbano makali kati ya viongozi wa Chadema, Bunge na Serikali.

Mzozo ulianzia Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wakati Lissu akipatiwa huduma ya kwanza. Serikali ilitaka apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), lakini viongozi wa Chadema walitaka akatibiwe Nairobi, Kenya, jambo lililotekelezwa kwa kuchangishana fedha za kukodisha ndege na kugharamia matibabu.

Malumbano hayo yameendelea kuchukua sura mpya kila siku, huku kila upande ukivutia kwake, kunyoosheana vidole na kujitetea kwa kila namna.

Miongoni mwa viongozi wa Chadema aliyeshiriki kumsaidia Lissu tangu hospitalini hadi Nairobi ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ambaye amerudi nchini hivi karibuni.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, Msigwa anasimulia hatua kwa hatua kuhusu misukosuko ya tukio hilo na safari ya kwenda Nairobi ilivyokuwa. Endelea

Swali: Tumesikia mambo mengi kuhusu mkasa uliompata Tundu Lissu hivi karibuni. Kwa kuwa wewe ulikuwapo tangu Dodoma na sasa umetoka Nairobi, hebu tueleze hali ilikuwaje wakati huo na sasa ikoje?

Jibu: Nataka tu niwaambie Watanzania kwamba Tundu Lissu wetu aliumizwa sana katika jaribio la kuchukua uhai wake. Watu wasichukulie kama ni jambo dogo, ni jambo kubwa lililoharibu hata akili za watu tuliokuwa karibu naye.

Mimi ambaye nilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuwa naye, nikafika mahali nikaona risasi siiogopi tena kwa maumivu aliyokuwa nayo. Nisingependa kama Taifa tufikie huko, yaani tusiogope risasi.

Hali aliyokuwa nayo hata alipofika Nairobi, madaktari walishangaa kuona Lissu akiwa hai kwa sababu alipoteza damu nyingi sana. Lakini, niwashukuru sana madaktari wa Hospitali ya Dodoma kwa huduma waliyotoa kufanya Lissu tufike Nairobi.

Swali: Hali ilikuwaje baada ya kupata ndege na kuanza safari ya Dodoma.

Jibu: Kwenye ndege nako tulipata shida kidogo, kuna wakati kitanda kilifyatuka. Mimi nikawa nashikilia, Mwenyekiti kuna hewa ya Oxygen alikuwa anashikilia ambayo ilikuwa imetoboka, kwa hiyo muda mrefu mimi nimeshikilia kitanda, madaktari wale nao wameshikilia.

INATOKA UK 15

Height (kimo) ya ndege nayo ilikuwa ndogo na (Lissu) alikuwa apewe dawa za usingizi, inakuwa siyo rahisi, hewa na maji ilikuwa inashindwa kufika vizuri.

Kwa hiyo kisaikolojia unaathirika kwa kuona mateso aliyopata. Lakini, tulifika Nairobi vizuri wametupokea wakaanza kushughulika naye, mpaka mambo yakaenda vizuri. Lakini, niseme mwenzetu ameumizwa sana.

Leo (Jumatano) ndiyo nimeondoka Nairobi na nilipata nafasi ya kumuaga, anaendelea kupata operesheni za hapa na pale. Isingependeza kuingia kwa undani kwa ajili ya kulinda privacy (faragha) ya mgonjwa. Lissu anaendelea vizuri, yuko critical lakini stable, kiasi kwamba anaanza kupata vitu vya majimaji.

Swali: Awali Serikali ilishauri Lissu atibiwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa nini ninyi mling’ang’ania kwenda Nairobi?

Jibu: Tulipomwondoa hapa, hatukusema kuwa madaktari wetu hawawezi, sababu kubwa ni security (usalama). Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa hospitali ya Muhimbili haina tofauti na hospitali ya Jomo Kenyatta kule Kenya ambayo nayo ni ya Serikali, lakini hospitali tuliyompeleka siyo ya umma, ina gharama kubwa lakini ina huduma kubwa.

Huduma zinazidiana. Ukienda Afrika Kusini, ukienda Ulaya au Marekani, kuna utofauti. Kama tutalazimika kwenda nje baada ya kushauriana na madaktari, lazima tutumie ndege ua kubeba wagonjwa, haitakuwa chini ya Dola 250,000. Hiyo ni mikakati tunayofanya.

Pamoja na maombi, kilichosaidia pale ni kwamba wenzetu Nairobi wana vifaa vya kisasa ambavyo vinacheki maeneo mengi sana. Kwa hiyo utaona lile jopo la madaktari 10, wengine ni wa mifupa, wengine wa saikolojia, wengine wa ndani ya tumbo na maeneo mengine, wote wanakaa kumhudumia.

Sasa tulikuwa tunashangaa, tuna wataalamu wengi hapo Muhimbili, lakini hatuna vifaa vya kutosha na madaktari kimekuwa kilio chao kikubwa. Lissu yuko katika hali ya dharura, unasema tufuate utaratibu, kwamba aende Dar es Salaam, madaktari wakae kwanza.

Alipofika Nairobi, kila kitu kilisimama, tulikuta pameandaliwa vizuri kwenda hospitali. Maana yake si kwamba wanaanza tu kuunga mifupa. Wakafanya vizuri, sasa ndiyo wakasema wanampeleka kwenye chumba cha upasuaji.

Swali: Pengine huo ndiyo utaratibu wenu wa matibabu bungeni au Serikali, kwa nini msingeufuata?

Jibu: Kwa kweli huduma ya kwanza aliyoipata Dodoma ilikuwa nzuri sana. Sasa ndiyo useme tufuate utaratibu? Ni mawazo ambayo naweza kusema yalikuwa ya kijinga.

Nadhani ni maneno katika kitabu cha No longer at ease, mwandishi anasema kuku akienda porini akakamatwa na mbweha, akiwa kwenye kinywa cha mbweha, huanzi kumkemea kuku kwamba kwa nini ulikwenda porini, unamtoa kwanza kisha unamwambia usiwe unakwenda porini utaangamia.

Sasa Lissu yuko kwenye hatari ya kupoteza uhai, watu wanasema tufuate utaratibu? Hata Kenya wanatushangaa wabunge wa Tanzania, kwamba Watanzania tuna bima inayofanya kazi tu ndani, wanasema ninyi VIP wa aina gani?

Wanashangaa Wakenya. Wakati wa Anna Makinda tulikuwa na bima ya Jubilee, lakini sasa hii ni ya ndani. Tunafikiria bora tukate bima ya binafsi, kwa sababu hatuko salama.

Ukiangalia wenzetu Kenya, mbunge analindwa na Serikali, walinzi zaidi ya wanne ambao wako full armed (wenye silaha), lakini na nyumbani wako wawili, kwa sababu huyu ni mbunge anayeisimamia Serikali, anakosoa. Halafu mtu anakwambia uende Muhimbili.

Swali: Hivi karibuni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali iko tayari kumtibu Lissu mahali popote duniani kama familia yake itaomba, kwa nini msiombe?

Jibu: Sisi hatuhitaji kuiomba Serikali, inawajibika kumtibu Mbunge. Bunge linawajibika kumtibu Mbunge, lakini kwa sababu Spika ametishwa, Bunge halifuati utaratibu. Hebu tufikirie, kosa la Lissu ni nini katika nchi tukiwa wakweli?

Tunasimama kwenye jukwaa, tukamate kipaza sauti, tunawaambia Serikali imekesea moja, mbili, tatu… tunawaambia bombardier (ndege ya Serikali) imekamatwa, wawekezaji wanaondoka, sisi tunaisaidia Serikali, sisi ni marafiki.

Serikali inapaswa iwalinde hawa watu wanaoisaidia Serikali.

Swali: Ile kauli yako kwa Spika Job Ndugai kuhusu nani aliyelipia ndege huoni kwamba ilikuwa mapema mno kuitoa?

Jibu: Ulikuwa ni wakati mwafaka kwa sababu niliona Spika analeta utani kwenye masuala ya msingi. Ni kweli yule bwana alisaidia sana wakati tunatafuta ndege, kwa sababu ile ndege iliyoletwa ilikuwa haiwezi na ilibidi tutafute ‘jet’.

Ni kweli yule bwana (Turki) alitusaidia lakini hakulipa. Sasa Spika anasema amelipa wakati hakulipa. Kama amelipa kwa nini watuletee sisi invoice? Nasema hivyo kwa sababu niko kwenye Tume ya Bunge.

Spika hana uwezo wa kuliendesha Bunge, ndiyo maana nimesema, akitaka anifukuze hata kesho. Kimsingi Tanzania hatuna Bunge huru. Kwa mimi ambaye nimetoka Kenya, ukiangalia jinsi wenzetu wanavyofanya kazi kwa uhuru, jinsi vyombo vya habari vinavyofanya kazi, utafikiri uko Ulaya, kweli.

Jana nimeona watu wameandamana mpaka mahakamani, japo walizidisha kugonga milango ya mahakama, lakini polisi waliwaacha. Kesho wataandamana Nasa yataisha. Watakuwa na Uhuru pale watamkosoa, mambo yanaendelea. Watu wamewekeza vizuri, kuna uchumi mzuri.

Sasa hapa, huko mitaani watu mnateta na hii hali msidhani kwamba kuna mtu atakuja kuwabadilishia hapa Tanzania, ni sisi wenyewe. Tuwe huru, Msigwa niwe na uwezo wa kukosolewa na kila mtu akosolewe.

Kwa hiyo kauli yangu ilikuja wakati mwafaka na nina maanisha, niko tayari kufukuzwa bungeni, kwa sababu Spika asidhani kwamba hatuwezi kuishi bila kuwa wabunge. Siyo kwamba uanasiasa wangu utakoma kwa sababu siko ndani ya Bunge.

Wala asidhani kwamba tutakosa hela, mimi kwa sasa nina miaka 52, hapo bungeni si nina miaka saba tu? Miaka yote hiyo nilikuwa naishije? Kwa hiyo haitatufanya tunyamaze.

Swali: Kwa nini mnaoikosoa Serikali halafu mnalalamika kwamba haiwajali katika suala hili?

Jibu: Wana hiari ya kuja, maana yake kupigwa risasi siyo jambo la mchezo, unakufa kabisa. Sisi ndiyo tunapigwa risasi. Sasa hizo ni hisia tu, wangekuja kumuona wakafukuzwa hiyo ingekuwa kweli.

Kweli mtu kama Lissu ni mtu wa Rais John Magufuli kutoa masikitiko yake kwenye Twitter?

Angekuwa Mbunge wa CCM wange tweet kama hivyo? Ni mtu wa ku-tweet masikitiko yake hivyo? Ni mtu ambaye mpaka leo hakuna hata mtu aliyekamatwa? Magari yametajwa yanaeleweka.

Pale anapokaa Lissu ni karibu na anapokaa Naibu Spika anayelindwa na askari wenye silaha, wanakaa viongozi, mawaziri.

Tuliwauliza waendesha bodaboda wakasema, pale mliofika mnapajua, walizuia njia ile ya Dodoma Klabu 84 na huku (kwenye tukio), walipomaliza mipango yao walifungua.

Swali: Kwa hiyo kuna watu mnawahisi?

Jibu: Sisi tunaihisi Serikali.

Swali: Lakini si mtu moja kwa moja?

Jibu: Nimesema, hivi wakitaka kujua kama mimi niko hapa, hawatajua? Kwa sababu wale watu waliokwenda pale walikuwa wanawasiliana na kuna mnara pale. Hiyo ni akili ya kitoto tu. Ukicheki mawasiliano lazima utawajua. Kilichomwokoa Lissu ni kwa sababu hakushuka kwenye gari.

Swali: Kuhusu dereva wa Lissu, mbona mmempeleka Nairobi wakati anatafutwa na polisi?

Jibu: Wao walisema amekimbia, ngoja niulize swali, polisi wamekuja hospitali saa mbili baada ya tukio. Mimi nilikuwa mbunge wa kwanza kufika hospitali, nilifungua kwa nguvu kwenye huduma ya kwanza, baadaye wakaja kina Mbowe (Freeman) na Selasini (Joseph), hata waandishi wa habari walichelewa.

Nilikuwa mtu wa pili kupata taarifa, nikaendesha gari mwenyewe mpaka kufika pale ndani. Shughuli zote zimekwisha, polisi wamekuja baada ya saa mbili.

Pili, hata kwenye tukio la Lissu kupigwa risasi, walikuja baadaye sana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad