Wakuu wa mikoa na wilaya wametakiwa kusimamia kikamilifu upatikanaji wa dawa, vifaa tiba kuanzia kwenye Zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini ili wananchi wapate huduma bora.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala alipokuwa akifungua majengo ya kutoa huduma ya afya ya uzazi katika Zahanati 26 mkoani Kigoma, shughuli iliyofanyika kijiji cha Mwakizega, wilaya ya Uvinza katika mkoa wa Kigoma hivi karibuni.
Amesema serikali imetenga Sh269 bilioni kwa ajili ya kununua dawa mwaka huu ambapo mwaka 2015 kiasi kilichotengwa kununua dawa ilikuwa Sh31 bilioni.
Shirika la Engender Health limejenga majengo 26 ya kutoa huduma ya afya ya uzazi yenye uwezo wa kutoa huduma ya uzazi na upasuaji wa dharura pindi inapohitajika kwa vile baadhi ya wilaya hazina hospitali za wilaya ambazo ni ngazi ya rufaa kwa wagonjwa wanaotoka kwenye vituo vya afya na zahanati.
“Vifo vya kinamama na watoto lazima vipungue kuanzia ngazi ya familia, jamii, vituo vya kutoa huduma ya afya kwa sababu kama kila mmoja atakuwa makini kufuata maelekezo ya wataalamu ni wazi vifo vitapungua, maana asilimia 19 ya vifo vinavyotokana na uzazi chanzo ni kuharibika mimba,” amesema Dk Kigwangala
Amesema mkoa wa Kigoma kuna vifo 248 katika kila vizazi hai 100,000 ambapo chanzo chake ni kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua na ukosefu wa damu.
Naibu mwakilishi mkazi wa EngenderHealth Tanzania, Lulu Ng’wanakilala amesema mradi huo ulihusisha ujenzi wa Zahanati mpya 24 na ukarabati wa nyingine mbili zilizogharimu Sh2.749 bilioni, huku vifaa tiba vikigharimu Sh612.5 milioni.
Alisema watoa huduma 417 walipata mafunzo ya kuhudumia kinamama wajawazito ambapo wengine 156 walifundishwa jinsi ya kuhudumia na kutoa elimu vijana 10,700 mkoani Kigoma.
Mwakilishi wa Bloomberg Philanthropies nchini, Dk Godson Maro amesema wataendelea kutoa ufadhili kwenye miradi ya afya mkoani Kigoma ambapo lengo ni kufikia asilimia 75 ya kinamama wanaojifungua katika vituo vya huduma ya afya ifikapo mwaka 2019.
Vifo zaidi ya 100 vinavyotokana na uzazi vimezuiliwa na magonjwa ya kuambukiza yamepunguzwa kutokana na kuboreshwa kwa huduma ya afya katika ngazi ya zahanati hadi hospitali za juu.
“Hadi sasa kinamama 5,000 walijifungua katika vituo vya huduma na mimba 289,217 zisizopangwa zilizuiliwa, lakini pia mimba zaidi ya 89,000 hazikuharibika kama ilivyokuwa awali huduma ilipokuwa haijaboreshwa,” alisema Dk. Maro.
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma, Dk Fadhil Kibaya amesema hadi kufikia Mei mwaka huu asilimia 76 ya dawa zilipatikana ambapo lengo la kitaifa ni asilimia 80.