Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM) mchana wa leo Septemba 26, 2017 amefanikisha safari ya mgonjwa Bw. Samson Mwanga mkazi wa kijiji cha Mipilo Singida Kaskazini anayeishi Manyara ambaye amepasuka mishipa kichwani na kuwaishwa KCMC.
Lazaro Nyalandu amesema kuwa ndege iliyotumika kumbeba mgonjwa huo imetoka nchini Kenya hivyo amewashukuru madaktari na wafanyakazi wa hospitali ya Rufaa ya Hydom kwa utumishi wao kumuhudumia mgonjwa huo wakati wakisubiri mgonjwa huyo kusafirishwa kwa matibabu zaidi ili kuokoa maisha yake.
"Nimewasili uwanja wa ndege wa Hospitali ya Hyadom kwa ajili ya dharura ya kumsafirisha mgonjwa, Bw. Samson Mwanga, mkazi wa kijiji cha Mipilo, Singida Kaskazini, aishiye kijiji cha Gidika (Manyara) aliyepatwa na kupasuka mshipa kichwani na kusababisha kuhitaji kile madaktari walichokiita 'Immunogloblin Injections" ili kunusuru maisha yake. Tumempandisha ndege ya Shirika la "Flying Medical Doctors", iliyotokea Nairobi na kuwasili hapa Hydom mchana huu." alisema Nyalandu
Mbunge huyo aliendelea kuwashukuru madaktari hao
"Nawashukuru madaktari na wanafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Hydom kwa utumishi wao uliotukuka, na kwa kumhudumia mgonjwa Samson Mwanga hadi tukaweza kumpandisha ndege kwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Kilimanjaro mchana huu" alisema Nyalandu
Hii ni mara ya tatu kwa Mbunge huyu kufanikisha safari za wagonjwa kwenda kwenye matibabu mbalimbali alianza kwa kufanikisha safari ya watoto watatu walionusurika kwenye ajali ya gari ya shule ya Lucky Vicent jijini Arusha, akafanikisha kuwapeleka watoto wawili hospitali waliovunjika miguu kwenye ajali ya gari ya mizigo la mnadani na sasa amefanikisha safari ya mgonjwa huyu Samson.