Wiki mbili baada ya ofisi za mawakili ya Prime Attorneys jijini Dar es Salaam kuvamiwa usiku wa manane na watu wasiojulikana, ofisi nyingine ya mawakili imefanyiwa uhalifu wa aina hiyo mjini hapa.
Katika uvamizi wa ofisi za mawakili za Prime Attoneys ambao pia wanamteta mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji, wezi waliiba sefu ya fedha na nyaraka baada ya kumfunga kamba mlinzi.
Mmoja wa mawakili wa kampuni hiyo, Hudson Ndusyepo alisema katika uvamizi wa ofisi hizo zilizopo kwenye jengo la Prime House, Mtaa wa Tambaza, Upanga nyaraka za mfanyabiashara huyo hazikuibwa.
Wakati uvamizi wa ofisi hizo ukiacha utata, watu wasiojulikana walivunja na kuiba mali mbalimbali katika ofisi mbili za mawakili jijini Arusha tukio ambalo limeibua hali ya hofu na sintofahamu kwa baadhi ya mawakili.
Ofisi zilizovamiwa ni za Ideal Chambers iliyopo jengo la Blue Rock na Equality Attorneys yenye maskani yake katika jengo la Said Kondo zote zikiwa katikati ya jiji.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha kwa kifupi kuvamiwa kwa ofisi hizo akisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo.
Wakili Edmund Mgemela wa kampuni ya Equality Attornerys alielezea kuwa tukio hilo lilitokea mwezi uliopita ambapo mara baada ya kuwasili asubuhi alikuta mlango wa ofisi ukiwa wazi na umevunjwa.
Mgemela alisema baada ya kuingia ndani alikuta baadhi ya nyaya za kompyuta ofisini zimenyofolewa, baadhi ya nyaraka zimechukuliwa sanjari na suti ambazo huzihifadhi ofisini kwake pia hazikuzikuta.
Hatahivyo, alisema kwamba aliripoti tukio hilo polisi na kupewa RB namba 790/2017 akiamini wahusika walikuwa na nia ovu kwa kuwa ndani ya jengo analofanyia shughuli zake kuna ofisi mbalimbali ambazo hazikuguswa siku ya tukio. “Mpaka sasa sielewi kama ni visasi au la, lakini ninachoweza kusema ni kwamba hawa watu walikuwa na nia ovu haiwezekani ndani ya jengo hili kuna ofisi nyingi wazipite zote kuanzia ghorofa ya kwanza mpaka wafike ya tatu kwangu na kuvunja,” alisema Mgemela.
Wakili kutoka Ideal Chambers, Robert Akileti alisema uvamizi katika ofisi yao ulifanywa Agosti 10 ambapo watu hao walivunja mchana alipokuwa ameenda kupata mlo.
Akileti alisema kuwa aliporejea ofisini kuendelea na shughuli zake alikuta mlango wa ofisi umevunjwa na kompyuta tatu mpakato (laptop)zimeibiwa kitendo ambacho kiliwapa hofu na mpaka sasa hawaelewi watu hao walikuwa na nia gani.