Ofisi ya mawakili ya Prime Attorneys imevamiwa usiku wa manane na watu wasiojulikana ambao wameiba kasiki lenye fedha na nyaraka.
Mmoja wa mawakili katika ofisi hiyo, Hudson Ndusyepo amesema ofisi yao imevunjwa na tayari ameenda polisi kutoa taarifa.
Kabla ya wizi huo, Ndusyepo ambaye ni miongoni mwa mawakili wanaomtetea mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji katika kesi ya uhujumu uchumi, amesema kabla ya wizi huo, waliohusika walimfunga mlinzi kwa kamba.
Kampuni ya Prime Attorneys katika tovuti yake inaeleza ilianzishwa mwaka 2010.
Ofisi za kampuni hiyo zipo jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza, Upanga jijini Dar es Salaam.
Ofisi hizo zipo kwenye jengo la ghorofa tano lililopo jirani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala.
Awali, asubuhi mwandishi wa Mwananchi alishuhudia barabara ya kuingia eneo hilo ikifungwa kwa muda na polisi ambao walitumia magari yao kuziba njia na kuweka uzio wa utepe wa rangi ya njano.
Jengo la Prime House lina ofisi za kampuni mbalimbali, zikiwemo za mawakili, duka la dawa na sehemu ya kufanya mazoezi gym.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea kati ya saa nane na saa tisa usiku wa kuamkia leo Jumanne.
"Kwa sasa siwezi kusema wahalifu hawa walilenga ofisi gani maana zipo nyingi katika jengo lile. Naomba mtupe nafasi tufanye uchunguzi kisha tutawapa taarifa," amesema Kamanda Hamduni.