Pendekezo la Kiutu Kwa Viongozi Wetu wa Kisiasa Kuhusu Tundu Lissu

Nianze kwa kuyarudia maneno yangu ya awali kuhusu madhila yaliyomkumba Tundu Lisu.

Mimi sijui ni nani aliyemdhuru Bw. Lisu. Ila najua kuna watu wengi walio na nadharia zao juu ya nani ni mhusika. Ni haki yao kudhani wanachodhani na kuamini wanachoamini.

Ambacho ningependa kukiona kutoka kwa viongozi wetu ni kuweka tofauti zao za kiitikadi pembeni.

Itakuwa ni vyema pindi Bw. Lisu arudipo nchini kwa rais Magufuli kumtembelea na kumjulia hali. Kama yeye rais Magufuli hahusiki hata kidogo na kilichomtokea Bw. Lisu, kama dhamiri yake ni safi kabisa, basi itakuwa ni jambo jema sana akienda kumjulia hali na kumpa pole.

Na hilo lisiishie kwa rais Magufuli tu. Hata marais wastaafu na viongozi wengine waandamizi wa CCM, kama hawakuhusika kwa namna moja ama nyingine katika huo mpango wa kumdhuru Bw. Lisu, kama dhamiri zao ziko safi kabisa, basi nao nawasihi waende kumjulia na kumpa pole.

Vilevile, Bw. Lisu pamoja na CHADEMA wenzake, kama na wao hawajui kwa uhakika ni nani aliyepanga mpango huo, ni vizuri wakakubali kuwapokea hao viongozi wa CCM wataokuja kumjulia hali.

Kufanya hivyo kutatuma ujumbe murua kuwa hata kama kuna tofauti kali za kiitikadi baina ya pande hizo mbili, tofauti hizo haziwezi kuuzidi utu.

Utu wetu ni tunu ambayo hatuna budi kuienzi. Bila utu hatuna jamii. Hivyo ni vyema kwenye mambo yahusishayo uhai na/ama kifo ni vyema tukautanguliza utu wetu na kuziweka tofauti zetu za kiitikadi nyuma.

NB: Natambua mpo ambao mnaona kwa rais kufanya hivyo nilivyopendekeza ni unafiki. Ni haki yenu kuona mnavyoona.

By Nyani Ngabu

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad