Watu wawili wamekufa kwa kupigwa risasi na askari polisi baada ya kuibuka mzozo kuhusu ng’ombe waliokamatwa katika Kijiji cha Nyalutanga wilayani Morogoro.
Pia, imeelezwa mtu mmoja amejeruhiwa kwa risasi kwenye makalio na ng’ombe 35 wameuawa na zaidi ya 40 kujeruhiwa katika mzozo huo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa amethibitisha vifo vya watu hao wawili, akisema hana taarifa kuhusu aliyejeruhiwa.
Dk Kebwe amesema mzozo huo umeshapatiwa ufumbuzi na waliokufa katika tukio hilo wamezikwa leo Jumanne, huku uchunguzi ukiendelea kuhusu wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kumshambulia kwa mawe askari aliyefika kutuliza mzozo huo.
Mkuu wa mkoa amesema ameunda kamati kuchunguza tukio hilo ambalo lilisababisha askari kufyatua risasi hewani kuwatawanya wananchi waliokuwa wamemzonga na kwa bahati mbaya risasi ziliwapata watu wawili.
Amesema watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria. Pia, amewaonya wafugaji wanaoacha mifugo ikizurura ovyo.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyalutanga kilichopo Kata ya Kisaki, Said Masongele amesema mzozo huo ulitokea jana saa saba mchana katika eneo la ofisi za serikali ya kijiji.
Masongele amewataja waliofariki dunia kuwa ni Ramadhan Kiwenge na Kibwana Msipwile.
Amesema mkazi mwingine Ismail Msagule amejeruhiwa kwa kupigwa risasi kwenye makalio na amelazwa katika zahanati hiyo.
Mwenyekiti huyo amesema hilo lilitokea baada ya mifugo kuingia shambani kwenye bonde la Kikwato na kukamatwa na mgambo na walinzi wa jadi (Sungusungu).
Amesema awali, viongozi wa kijiji wakiwa kwenye kikao walipata taarifa kwamba kuna mifugo imevamia mashamba, hivyo walitumwa mgambo kwenda kuikamata.
Muda mfupi baadaye amesema alipokea simu ikieleza Mohamed Kassim alijeruhiwa kichwani na mfugaji wakati wa kukamata mifugo.
Mgambo wa kijiji hicho, Kibwana Mbegu aliyeshiriki kukamata mifugo amesema watu hao watatu walifyatuliwa risasi wakati askari akijihami baada ya wananchi kujaribu kupora silaha.
“Tulikamata mifugo isiyopungua 80 katika mashamba ya Kikwato ikila mazao, wakati tukifanya hivyo mwenzetu alijeruhiwa kwa kupigwa fimbo kichwani na mfugaji. Tuliwazidi nguvu wafugaji na kuswaga mifugo hadi ofisi za kijiji kwa hatua za kisheria,” amesema Mbegu.
Mbegu amesema baada ya dakika chache, wafugaji walifika ofisi za kijiji wakiwa na silaha za jadi, wakati huo wananchi wakiwa wanakusanyika huku kukiwa na askari polisi mwenye silaha kulinda amani eneo hilo.
Amesema baada ya wafugaji kufika eneo hilo, walianza kuchukua mifugo kwa nguvu jambo lililosababisha askari kufyatua risasi hewani kuwatawanya.
Mbegu amesema baadhi ya wananchi walimfuata askari kwa lengo la kumnyang’anya silaha, huku wengine wakirusha mawe.
Amesema askari alifyatua risasi ili kuwazuia ambazo ziliwapata watu wawili na baadaye alikimbia eneo hilo.
Mgambo huyo amesema kundi la wananchi lilimkimbiza ndipo alipofyatua risasi nyingine iliyomjeruhi mwananchi mwingine kwenye makalio.
Amesema askari huyo alijificha ndani ya nyumba kijijini hapo na alipiga simu kituo cha polisi Kisaki Gomero kuomba msaada kwa wenzake waliomuokoa katika eneo hilo ambalo lilikuwa limezingirwa na wananchi.