Hatua hiyo inakuja baada ya Waziri mkuu kutoa agizo kutokana na malalamiko ya Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba kuwa wawekezaji hao kutoka China wanaendesha shughuli za uchimbaji bila ya kuwa na kibali.
Ambapo Mgumba alieleza kuwa tangu mwaka 2010 wawekezaji hao wameendesha shughuli zao bila kulipa kodi za Serikali na tozo za halmashauri, hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Mbunge huyo ambaye machimbo hayo yako jimboni kwake, alisema licha ya uongozi wa mkoa kwenda eneo hilo na kuizuia kampuni kuendelea na uchimbaji hadi itakapopata vibali ilikaidi na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Majaliwa alisema iwapo wahusika watabainika kuwa hawajafuata sheria, kanuni na utaratibu hatua zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika eneo hilo chini ya ulinzi na kuwasiliana na ubalozi wa China nchini.
Hatimae, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt Stephen Kebwe alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kuwakamata raia hao na kuamuru warudishwe nchini kwao baada ya kugundulika wanafanya kazi bila kufuata utaratibu,sheria, na kanuni za nchi.