Rais John Magufuli amerejea agizo lake la kupiga marufuku mfanyakazi yeyote kuhamishwa kituo cha kazi pasipo kulipwa stahiki zake.
Ametoa agizo hilo leo Jumatatu, baada ya kusikiliza kero za wananchi wakiwemo wafanyakazi waliolalamika kuhamishwa vituo vya kazi bila kulipwa stahiki zao.
Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Sangsi nje kidogo ya Jiji la Arusha na wa Pacha ya Kia akiwa njiani kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara ya siku sita mkoani Arusha.
Akizungumzia kero za wananchi wa Pacha ya Kia waliolalamikia tatizo la uhaba wa maji, kunyang’anywa maeneo ya biashara na waliokuwa walinzi wa uwanja wa ndege kudai haki zao, Rais Magufuli ameziagiza mamlaka husika kushughulikia matatizo hayo.
Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua kero za wananchi na kuwahudumia bila kuwabagua kwa misingi ya itikadi za kisiasa, dini na ukabila.
Amesema katika kutimiza azma hiyo, Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Usa River - Arusha inayojengwa kwa gharama ya Sh139 bilioni; mradi wa maji wa Arusha utakaogharimu Sh42 bilioni; mradi wa kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 200 na mingine inayotekelezwa katika maeneo hayo.
“Nina uhakika ninyi wakazi wa Arusha mnaona inavyobadilika, kabla ya kujengwa barabara hii kulikuwa kunatokea ajali nyingi na kuna watu walikufa pale kwenye daraja, inawezekana wengine wameanza kusahau, wanaozaliwa sasa hivi wanaweza kuona haya si chochote lakini hii ni ishara ya kupanda kwa uchumi wetu, uchumi unapopanda na miundombinu inakuwa mizuri,” amesema.