Rais Mugabe Amshambulia Trump

Rais Mugabe Amshambulia Trump
Rais Robert Mugabe amemshambulia Rais Donald Trump wa Marekani katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa akimkejeli kuwa sawa na sanamu kubwa la Goliath lililonakshiwa kwa dhahabu.

Akihutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) ambako shutuma za viongozi wengine hazikulenga mtu binafsi, kiongozi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93 alimsuta Trump kwa sera zake na mwonekano wake.

"Baadhi yetu,” alisema Mugabe na kusita kidogo kuweka msisitizo “tulikerwa sana kama si kuogofywa na kile kilichoonekana ni kurejea kwa “Goliath Mkubwa wa Dhahabu” aliyetajwa kwenye biblia.

Katika Biblia Takatifu, Goliath anatajwa kuwa alikuwa askari mkubwa, mwenye nguvu na kiongozi madhubuti wa jeshi, lakini aliuawa kwa jiwe lililorushwa kwa silaha dhaifu aina ya kombeo tena na kijana mdogo Daudi.

"Je, tunaye Goliath wa kwenye biblia miongoni mwetu, ambaye anatishia kuzifuta nchi nyingine kwenye uso wa dunia?" alihoji Mugabe kauli iliyoamsha watu kumshangilia kwa nguvu kwenye ukumbi huo huku wanadiplomasia wawili wa Marekani wakisikitahayari.

"Na labda nitoe wito kwa Rais wa Marekani kwamba Bwana Trump tafadhali piga tarumbeta kunakshi muziki wa kuelekea kuimarisha tunu za umoja, amani, ushirikiano, mshikamano, majadiliano ambazo mara zote tumekuwa tukisimamia na ambazo zimeandikwa vizuri katika waraka wetu unaoheshimika sana, Katiba ya Umoja wa Mataifa.”

Trump aliwashangaza watu wengi katika UN Jumanne iliyopita aliposimama kwenye jukwaa kutishia “kuiangamiza” Korea Kaskazini huku akimwita kiongozi wake Kim Jong-Un kuwa "Rocket Man" yaani Mzee wa Maroketi.

Kwa muda mrefu Mugabe ana uhusiano mgumu na nchi za Magharibi ambazo zimemwekea vikwazo vya kiuchumi kushinikiza demokrasia katika nchi yake aliyoiongoza kwa miaka 37 sasa.

Katika hotuba hiyo, vilevile Mugabe alipaza sauti hasa kuhusu mipango ya Trump kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa Paris unaohusu mabadiliko ya tabia nchi.

Mugabe alihimiza ushirikiano "kwa lengo la kuzuia mwenendo usiofaa utakaosababisha uharibifu wa mazingira ambayo sote tunategemea kwayo”

 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad