Mwendesha mashtaka wa kesi za ufisadi nchini Brazil amemfungulia mashtaka rais Michel Temer kwa kosa la kuzuia sheria kuchukuwa mkondo wake na kuhusika katika mtandao wa rushwa.
Hatua hiyo ni ya pili katika kesi ya jinai inayomkabili rais huyo ambaye amekanusha madai hayo.
Wanamtuhumu bwana Temor kwa kuchukua hongo na kujaribu kuwanyamazisha mashahidi.
Bwana Temer amepinga madai ya kufanya makosa yoyote.
Mashtaka ya awali ya ufisadi yalizuiwa na bunge la uwakilishi ambalo lina uwezo wa kuamua iwapo rais anafaa kufunguliwa mashtaka au la.
Katika shtaka la pili rais Temer ameshtakiwa pamoja na washirika wake sita wa kisiasa.
Kiongozi wa mashtaka Rodrigo Janot alisema katika taarifa kwamba bwana Temer alihudumu kama kiongozi wa genge la wahalifu linaloshirikisha wanachama waandamizi wa chama chake cha PMDB.
Amesema kuwa kundi hilo lilidaiwa kuchukua hongo ya takriban dola milioni 190 kwa lengo la kuwazawadi waliotoa fedha hizo kandarasi katika kampuni za umma.
Mashtaka hayo yanatokana na ushahidi uliotolewa na mmiliki wa kampuni kubwa ya nyama JBS Joesely Batista na Wesley Batista.