Rais wa Malaw Profesa Peter Mutharika amempongeza Rais Robert Mugabe akisema utajiri mkubwa wa historia umemfanya kuwa shujaa pekee aliyebaki wa kupigania utaifa barani Afrika.
Profesa Mutharika alisema mara zote amekuwa akifurahia kukutana kwenye vikao na Rais Mugabe ambaye amemwelezea kama “shujaa pekee aliyesimama” na akaongeza kuwa anajifunza mengi kutoka kwa mwana huyo wa Afrika.
Rais Mugabe na mwenzake huyo wa Malawi wako New York kuhudhuria mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lililoanza vikao vyake Jumanne.
Akizungumza baada ya kumtembelea Rais Mugabe hotelini kwake, kiongozi huyo wa Malawi alisema Malawi na Zimbabwe zina historia ndefu ambayo haiwezi kusahaulika.
“Tulizungumzia juu ya Malawi na Zimbabwe. Historia ndefe. Unafahamu Rais Mugabe ni kaka yangu. Rais wa zamani wa Malawi na mimi mwenyewe tumefanya kazi kwa upendo mkubwa.
“Zimbabwe na Malawi ni kama nchi moja. Hakuna mgogoro, hakuna mvutano wowote. Urafiki wetu ni asilimia 100,” alisema Profesa Mutharika.
“Nitapenda kwenda Zimbabwe nay eye pia anapenda kuja Malawi. Tumezungumzia juu ya kuendelea kubadilishana ziara katika siku chache zijazo,” alisema.
Kuhusu mikutano yake na Rais Mugabe alisema: “Mara zote huwa najifunza kutoka kwake. Unajua ana utajiri mkubwa wa historia. Huyu ndiye shujaa pekee aliyebaki wa kupigania utaifa wa Afrika na mapambano ya kudai uhuru. Ni kiongozi pekee aliyebaki amesimama. Ana utajiri mkubwa wa historia ya Afrika.
“Kila tunapokutana najifunza mengi kutoka kwake. Yeye huwa anatupatia mtazamo wa wapi tumetoka. Huwa nafurahishwa kukutana naye.”
Kiongozi huyo wa Malawi amezipuuzilia mbali nchi za Magharibi zilizokuwa na matarajio ya kumtumia kuvuruga uhusiano kati ya Malawi na Zimbabwe. Badala yake amezungumza kwa uwazi kuhusu uhusiano mzuri na kiongozi mwenzake wa Zimbabwe.