SERIKALI imekazia msimamo wake wa kutowapeleka viongozi wa nchi na wabunge katika hospitali za nje ya nchi kwa ajili ya matibabu isipokuwa kwa idhini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), na sasa hata kwa Rais.
Msimamo huo ulitangazwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, katika hafla ya uzinduzi wa wodi za upasuaji wa watoto MNH jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza katika halfa hiyo, Waziri Ummy alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Lawrence Museru kutotishika dhidi ya kauli za wanasiasa wanaolazimisha kutibiwa nje.
"Mkurugenzi wa Muhimbili naomba usitishike, awe Rais, niwe mimi, awe mbunge, akiomba kwenda kutibiwa nje kama nyie mna uwezo wa kumtibia huo ugonjwa wake msitoe ruhusa, msituogope, simamieni taaluma yenu," alisema waziri huyo.
Kauli hiyo imetolewa wakati kukiwa na mvutano baina ya serikali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi, Kenya kutokana na kushambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Dodoma Septemba 7.
Katika mvutano huo, serikali inasisitiza itagharamia matibabu ya mbunge huyo ikiwa familia yake itafuata utaratibu iliouweka mwaka jana kwa maofisa wa serikali na viongozi kupata kibali MNH kutibiwa ughaibuni.
Januari 11, mwaka jana, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ikishirikiana na Wizara ya Afya ilitangaza masharti mapya kwa wafanyakazi na maofisa wa serikali kwenda kutibiwa nje ya nchi, ikifuta utaratibu uliokuwapo ambao ulikuwa rahisi kupata kibali cha kwenda kutibiwa ughaibuni.
Msemaji wa Wizara wa Afya, Nsanchris Mwamwaja, alisema mtu atakayetaka kwenda kutibiwa nje ya nchi, atalazimika kuidhinishiwa safari yake na jopo la madaktari bingwa wa MNH.
Mwamwaja alisema uamuzi huo umelenga kuondoa mwanya wa baadhi ya watumishi wa umma kwenda kutibiwa nje ya nchi kwa maradhi ambayo yanaweza kutibiwa kirahisi katika hospitali zilizopo nchini.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilikabidhiwa kwa Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 27 na baadaye kuwasilishwa bungeni mjini Dodoma Aprili 13, hadi Juni 30, mwaka jana, deni la serikali katika hospitali za rufaa za India lilifikia Sh. bilioni 19.193.
Kwenye ripoti hiyo, CAG Assad anazitaja hospitali za rufaa za India zinazoidai Tanzania kuwa ni Ahmedabad Sh. bilioni 2.056, Bangalore Sh. milioni 548.323, Chennai Sh. bilioni 6.164, Madras Sh. milioni 5.274, Hyderabad Sh. bilioni 2.594 na New Delhi Sh. bilioni 7.824 zinazotengeneza jumla ya Sh. bilioni 19.193.
Ripoti ya CAG kwa mwaka 2014/15 iliyowasilishwa bungeni Aprili 24, mwaka jana, ilionyesha kuwa mbali na kudaiwa Sh. bilioni 16.94 na hospitali za rufaa za India, Tanzania pia ilikuwa inadaiwa Sh. milioni 448.144 kwa ajili ya malipo ya matibabu ya nje ya nchi ya maofisa wa balozi mbalimbali.