Serikali imesema maiti zinazookotwa zikiwa zimetelekezwa uchunguzi unaonyesha wanaofanya hivyo ni wanaosafirisha binadamu kwa njia zisizo halali.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio tofauti ya miili ya watu kukutwa ikiwa imefungwa kwenye viroba na mingine ikiwa imefungwa mawe na kutumbukizwa mtoni na baharini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema kumekuwa na watu wanaosafirisha binadamu kutoka Somalia na Ethiopia kwenda Afrika Kusini kupitia Tanzania.
“Wamekuwa wakiwatupa baharini wanapokuwa wamekufa, kuna wengine 80 walitupwa wakiwa mahututi mpakani mwa Tanga na Bagamoyo na polisi walijitahidi kuwatengenezea uji mwepesi ili kuokoa kwanza uhai wao,” amesema.
Mwigulu amesema watu hao husafirishwa kama vile mizigo kwenye malori na wanapokufa kwa kukosa hewa miili yao hutupwa.
Akizungumza leo Alhamisi katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds, Mwigulu amesema kwa kuwa husafirishwa kwa njia haramu, wakishakufa miili yao hutupwa kwenye mito ili kukwepa kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Kumekuwa na matukio ya aina hiyo mara nyingi lakini wanaofanya biashara hiyo tumekuwa tukiwakamata na kuwafikisha mahakamani,” amesema.